MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma ya Nishati na Maji (Ewura) inakusudia kupunguza mwingiliano wa utendaji kazi baada ya kuanza kuweka mikakati kwa watumiaji wa huduma hizo, kufahamu wajibu wa kulinda miundombinu na kuboresha ufanisi wa kazi ili kuondokana na utendaji duni wa kazi, anaandika Moses Mseti.
EWURA imesema mikakati hiyo itasaidia kuleta utekelezaji wa majukumu na shughuli za kamati na baraza la watumiaji wa huduma za nishati na maji kutekeleza majukumu yao bila kuwepo changamoto zinazoweza kukwamisha utendaji wao wa kazi.
Mhandisi Thomas Mnunguli, Mwenyekiti wa Baraza la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Nishati na Maji, ameyasema hayo wakati wa ufunguzi wa mkutano wa tatu wa mwaka wa baraza hilo uliofanyika jijini Mwanza ulioshirikisha mikoa 18 kati ya 24 ya Tanzania bara.
Mhandisi Mnunguli, amesema kuwa mpaka sasa kazi walizotekekeza ni pamoja na programu za uelimishaji 408 zilizowafikia watu 26,007 ikilinganishwa na mafunzo mengine 46 yaliotekelezwa na kuwafikia watu 6,103 katika kipindi cha mwaka 2015/16.
Amesema kuwa, ni wakati muafaka wa mamlaka zinazotoa huduma kuzingatia sheria zilizopo ili kuweza kutoa huduma iliyo bora pasipo kuwa na upendeleo wowote kwa wateja wao ili kuondoa malalamiko yanayoweza kujitokeza.
Mnunguli amesema wanakabiliwa na changamoto kadhaa ikiwemo wajumbe wa kamati kutokuwa na mawasiliano hata pale wanapotumiwa taarifa, baadhi ya wajumbe kuwa nje ya mikoa yao ya kazi na kuzorotesha utekelezaji wa majukumu, kutokuwasilisha ripoti za kazi, kudai fedha za posho kwa kila kazi wanaposhiriki na mwamko mdogo wa kamati katika shughuli za uelimishaji na uhamasishaji.
“Wamejipanga kuongeza ufanisi, kujifunza, kubadilishana uzoefu na kukumbushana majukumu ya baraza na niwaombe wananchi kupaza sauti pale wanapoona haki yao inakiukwa kudai haki zao, kulipa bili na kujua utaratibu wa kuandika malalamiko yao pamoja na kulinda miundombinu,” amesema Mnunguli.
Mhandisi Goodluck Mmari, Katibu Mtendaji wa baraza hilo, amewataka washiriki kupenda kujifunza mbinu mbalimbali za kiutendaji katika kukabiliana na changamoto wanazokutana nazo ikiwemo kuelewa majukumu yao na ya wananchi huku ikiitaka Serikali kuendelea kuwekeza kwenye huduma za nishati na maji.
Leave a comment