August 17, 2022

Uhuru hauna Mipaka

EU ‘yamkazia’ Dk. Shein, JPM

Picha Kubwa, John Magufuli, Rais wa Tanzania akiteta jambo na Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein. Picha ndogo Seif Sharrif Hamad, aliyekuwa mgombea wa Urais Zanzibar kupitia CUF

Spread the love

TAARIFA kwamba Umoja wa Ulaya (EU) bado una msimamo kuwa, Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar uliofanyika 25 Oktoba 2015, ulivurugwa, imeamsha upya msisimko kwa umma wa Wazanzibari, anaandika Mwandishi Wetu.

“Hatua ya Umoja wa Ulaya kubaki na msimamo kwamba uchaguzi mkuu wa Zanzibar ulihujumiwa na lazima haki itendeke, inamaana kuwa dunia bado hairidhiki na dhulma iliyotendwa,” anasema mwanasheria anayefanya kazi za utetezi wa haki za binaadamu jijini Dar es Salaam.

Mwanasheria huyo ambaye ameshurutisha jina lake lisitajwe, amesema ni muhimu utawala wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ukaheshimu maamuzi ya wananchi kama walivyofanya kwenye uchaguzi uliopita.

Umoja wa Ulaya kupitia mwakilishi wake nchini Tanzania, Roeland van de Geer, umesema unaamini bado ipo haja ya serikali kusimamia kurudishwa kwa serikali ya mfumo wa Umoja wa Kitaifa (SUK) kwa kuzingatia masharti ya Katiba ya Zanzibar.

Amesema, msimamo wao unatokana na imani yao kuwa, uamuzi wa wananchi ndio unaopaswa kuamua mwelekeo wa nchi kisiasa ikiwemo muundo wa serikali, na sio vinginevyo.

Msimamo huo unachukuliwa kuwa ndio ufumbuzi muafaka wa mgogoro wa kisiasa unaoikumba Zanzibar kufuatia kufutwa kibabe kwa uchaguzi mkuu na matokeo yake yote.

“Inafurahisha kuwa dunia imeshikilia msimamo kutokana na kile ilichokiona siku ya uchaguzi. Hakuna ubishi kwamba uamuzi wa kufuta uchaguzi haukuzingatia msingi wa katiba na sheria.

“Ule ulikuwa ni uamuzi wa kisiasa uliofanywa kwa maslahi ya kikundi cha watu wasiofikiria hatima njema ya nchi,” amesema mwanasheria huyo.

Msimamo wa Ulaya ambao unaendana na mtizamo wa Marekani na mataifa mengine yanayofadhili Tanzania, umeamsha upya ari ya ulazima wa kuwepo mabadiliko Zanzibar.

Serikali iliyoundwa na Dk. Ali Mohamed Shein, ambaye alitangazwa mshindi wa urais ulipoitishwa uchaguzi mpya uliopewa jina la “uchaguzi wa marudio” hapo 15 Machi 2016, haijatambuliwa na jumuiya ya kimataifa, na bado kuna shinikizo kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano, Dk. John Magufuli kusimamia utaratibu wa kurudisha haki kwa wananchi.

“Tunatarajia ukichwa ngumu wa utawala wa CCM utasimamishwa na watu wao kuja kwenye ukweli kwamba uongozi uliopo Zanzibar hauna uhalali kisheria,” amesema mkazi wa Darajani mjini hapa.

Mkazi huyo ambaye ni mtumishi katika Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), amesema hujuma ya haki ya wananchi imechochea mvurugiko ndani ya sekta ya umma ambako watumishi hawana moyo wa kutumikia serikali tofauti na ilivyokuwa baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 2010.

Baada ya uchaguzi huo wa 2010, amesema japo mgombea wa upinzani, Maalim Seif Shariff Hamad wa Chama cha Wananchi (CUF), aliridhia matokeo ya kushindwa ingawa aliamini kuwa alishinda, iliundwa serikali ya umoja wa kitaifa ikimshirikisha yeye kama Makamu wa Kwanza wa Rais huku DK. Shein akimteua Balozi Seif Ali Iddi kuwa Makamu wa Pili

Hiyo ilikuwa ni hatua ya utekelezaji wa maamuru ya katiba iliyofanyiwa Mabadiliko ya Kumi Agosti 2010.
Utawala wa CCM unaolaumiwa kwa kuaminika kuwa ndio uliosimamia hujuma ya uchaguzi wa Zanzibar, uliunda serikali kwa kuteua viongozi kutoka chama hicho pekee ikishirikisha vyama viwili ambavyo havikufikisha hata asilimia 10 ya kura katika uchaguzi wa marudio.

CUF inayoshikilia kuwa ilishinda uchaguzi wa 25 Oktoba 2015, kwa kupata kura zaidi ya asilimia 52, imeongoza vyama vinginevyo vyote ukiacha AFP na TADEA vilivyoshirikishwa, kupinga serikali hiyo.
Wapinzani hao wakiwemo wagombea tisa wa urais katika uchaguzi wa 25 Oktoba 2015, hawaitambui serikali ambayo Soud Said Soud wa AFP na Juma Ali Khatib wa TADEA ni miongoni mwa wajumbe wa Baraza la Mawaziri.

error: Content is protected !!