May 29, 2022

Uhuru hauna Mipaka

EU, Marekani, Canada, Uswisi zajitosa kesi ya Mbowe

Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chadema

Spread the love

 

JUMUIYA za Kimataifa zimejitosa katika kesi ya ugaidi, inayomkabili kiongozi wa chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania cha Chadema, Freeman Mbowe na wenzake watatu. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Mbowe na wenzake watatu, Halfani Bwire Hassan, Adam Hassan Kasekwa na Mohammed Abdillahi Lingwenya, wanakabiliwa na tuhuma za uhujumu uchumi na kupanga njama za ugaidi.

Kesi hiyo ipo Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam, chini ya Hakimu Mwandamizi Thomas Simba.

Kesi hiyo ilikuwa inasikilizwa leo Alhamisi tarehe 5 Agosti 2021, kwa njia ya mtandao ‘Video Conference’ katika mahakama hiyo mbele ya Hakimu Mkazi Simba. Hata hivyo, haikuendelea baada ya kutokea tatizo la mtandao.

Wakati Marekani na Canada zikitoa matamko kuhusu kesi hiyo, Umoja wa Ulaya (EU) na Ubalozi wa Uswisi nchini Tanzania, mapema leo zilituma wawakilishi wake kusikiliza kesi hiyo, iliyoahirishwa hadi kesho Ijumaa tarehe 6 Agosti 2021.

Kabla ya kuahirishwa, wawakilishi hao walisikiliza kesi ya Mbowe na wenzake, iliyoendeshwa kwa lugha ya Kiswahili.

Mawakili wa Freeman Mbowe wakiwasili mahakamani Kisutu

Awali, Wakili upande wa utetezi, Peter Kibatala, alimuomba Hakimu Simba, aiendeshe kesi hiyo kwa lugha ya kingereza ili wawakilishi hao wa kimataifa waelewe mwenendo wake, lakini hakimu huyo alikataa pendekezo.

Hakimu Simba alikataa pendekezo hilo kwa maelezo baadhi ya washtakiwa wa kesi hiyo hawaelewi kingereza.

Hakimu huyo alichukua uamuzi huo baada ya kuwauliza washtakiwa hao, kama wataelewa endapo kesi hiyo itasikilizwa kwa kingereza, ndipo baadhi yao walijibu hawaielewi lugha hiyo.

Wakati EU na Ubalozi wa Uswisi nchini, zikituma wawakilishi wao mahakamani kufuatilia kesi hiyo, Ubalozi wa Canada nchini Tanzania, umesema unafuatilia kwa karibu mwenendo wake.

Taarifa za EU na Uswisi kutuma wawakilishi wake katika kesi hiyo, imetolewa na Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema, aliyesema “katika kesi hiyo, EU wametuma mwakilishi pamoja na Ubalozi wa Uswisi, walikuwa mahakamani kufuatilia. EU wametuma mwakilishi mmoja na Uswisi mmoja.”

Kupitia ukurasa wake wa Twitter, ubalozi huo umetoa wito kwa Tanzania, kufuata misingi ya kisheria ili kulinda misingi ya demokrasia nchini.

“Canada inafuatilia kwa ukaribu kesi dhidi ya mwenyekiti wa Chadema, Mbowe. Demokrasia imara inahitaji usawa na uwazi katika taratibu za kisheria kwa wananchi wote.”

Canada wamesema, haki za binadamu na uhuru wa kujieleza ni nguzo imara inayopaswa kutolewa kwa wanachi wote .

Wakati Ubalozi wa Canada ukitoa taarifa hiyo, jana Jumatano, Naibu Waziri wa Nchi wa Masuala ya Siasa wa Marekani, Victoria Nuland, alishauri Serikali ya Tanzania na vyama vya siasa vya upinzani, vitafute njia sahihi ya kumaliza mvutano huo, ili kuimarisha misingi ya demokrasia.

Nuland alitoa wito huo baada ya kuzungumza na Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan na baadaye kukutana na viongozi wa vyama vya upinzani nchini humo.

John Mnyika, Katibu Mkuu wa Chadema

Viongozi hao ni Zitto Kabwe, Kiongozi wa ACT-Wazalendo, John Mnyika ambaye ni Katibu Mkuu wa Chadema na Anthony Komu, Naibu Katibu Mkuu-Bara wa NCCR-Mageuzi.

Naibu huyo waziri Nuland alimshauri Rais Samia kuimalisha ulinzi na kutenda haki kwa wote bila kujadili itikadi zao za kisiasa.

Nuland alisema ana matumaini suala hilo la Mbowe litapatiwa ufumbuzi haraka kwa njia ya majadiliano kwa pande zote kuonyesha utayari.

Kwa mara ya kwanza Mbowe alipandishwa kizimbani tarehe 26 Julai 2021 na kusomewa mashtaka ya ugaidi, mbele ya Hakimu Simba. Hatua hiyo ilimuunganisha katika kesi hiyo ya ugaidi, inayowakabili wengine watatu.

Katika mashtaka hayo, Mbowe anadaiwa kula njama na kutoa fedha kwa ajili ya kufadhili shughuli za ugaidi. Inadaiwa alitenda makosa hayo kati ya Mei na Agosti 2020, kwenye Hoteli ya Aishi, Moshi mkoani Kilimanjaro.

error: Content is protected !!