Friday , 29 March 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Esther Matiko alivyolichambua Bunge la Makinda, Ndugai
Habari za SiasaTangulizi

Esther Matiko alivyolichambua Bunge la Makinda, Ndugai

Esther Matiko
Spread the love

ESTHER Matiko, Mbunge wa Tarime Mjini kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), amelichambua Bunge la 10 lililoongozwa na Anne Makinda na Bunge la 11 la Spika Job Ndugai. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam…(endelea).

Matiko amefanya uchambuzi huo leo Jumatano tarehe 1 Julai 2020 katika mahojiano maalum na MwanaHALISI Online.

Katika Bunge la 10 lililoongozwa na Spika Makinda, Matiko alikuwa mbunge wa viti maalum na Bunge hili linalomaliza muda wake la 11 la Spika Ndugai, Matiko alikuwa mbunge wa Tarime Mjini Mkoa wa Mara.

Akijibu swali la MwanaHALISI Online lililotaka kupata mtazamo wake wa Bunge la 10 na la 11 yeye akiwa yote ameyahudumu, Matiko amesema, “Bunge hili halikuwa huru, kama lilivyokuwa Bunge la 10.”

Matiko amesema, kuna masuala yanayolifanya Bunge la 11 kuwa na tofauti kubwa na Bunge la 10.

Ametaja baadhi ya masuala hayo ni, maazimio yaliyokuwa yanatolewa na Bunge la 10 chini ya Spika Makinda yalikuwa yanasikilizwa na Serikali, kuliko ilivyo kwa Bunge la Spika Ndugai.

“Katika Bunge la 11, ziliundwa kamati za kuchunguza madini, lakini ripoti zilienda Ikulu hazikuja bungeni kufanyiwa maamuzi,” amesema Matiko.

Baadhi ya kamati zilizoundwa na ripoti zake kukabidhiwa serikalini ni ya kuchunguza biashara ya madini ya Almasi; kamati ya kuchunguza utoroshaji wa Madini ya Tanzanite, ambayo ilitoa ushauri wa kujenga ukuta wa kilometa 25 katika Mgodi wa Mirerani, ambao Serikali iliutekeleza.

Spika wa Bunge la 10, Anne Makinda

“Bunge la 10 lilikuwa linarushwa mubashara (live), pamoja na maudhui yao kutohaririwa sana, tofauti na ilivyokuwa kwa Bunge la 11 huku suala lingine likiwa ni Serikali kuheshimu na kutekeleza maazimio yanayotolewa na Bunge,” amesema Matiko ambaye kabla ya kuingia kwenye siasa, alikuwa Mhadhiri Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM)

Amesema, masuala hayo hayakuonekana katika Bunge la 11 lililokuwa chini ya Spika Ndugai.

“Kuna utofauti mkubwa sana wa Bunge la 10 na 11, kwanza Bunge lilikuwa live (Mubashara). Kulikuwa na uhuru wa Bunge kusema na kuisimamia Serikali. Serikali ikiona kuna suala fulani bungeni, inasikiliza maazimio yanakuaje na inayatekeleza,” amesema Matiko.

Job Ndugai, Spika wa Bunge la Tanzania

Matiko ametolewa mfano maazimio yaliyotolewa na Bunge 10, kuhusu sakata la Operesheni Tokomeza, ambayo yalitekelezwa na Serikali, ikiwemo kuwachukulia hatua mawaziri kadhaa.

“Kuna kipindi kulikuwa na suala la operesheni tokomeza, watu walikuwa wakinyanyaswa. Tume iliundwa, ripoti ikasomwa bungeni na tuliazimia na na mawaziri wengi waliondoka.”

“Rais (mstaafu) Jakaya Kikwete alikuwa nje (ya nchi) lakini Waziri Mkuu (Mizengo) Pinda alimpigia simu akasema suala lishughulikiwe,” amesema Matiko.

Mawaziri waliong’olewa kutokana na ripoti hiyo ya Bunge kuhusu operesheni tokomeza ni; Khamisi Kagasheki wa Maliasili na Utalii, Dk Emmanuel Nchimbi (Mambo ya Ndani ya Nchi), Shamsi Vuai Nahodha (Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa) na Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk Mathayo David Mathayo.

Vurugu Bungeni
Moja kati ya vurugu zilizotokea Bungeni

Katika mahojiano hayo, Matiko amesema, Bunge la 10, hoja binafsi zilikuwa zinawasilishwa bungeni na kujadiliwa, lakini pia kulikuwa hakuna mfululizo wa adhabu kwa wabunge wa upinzani.

“Bunge lililopita, hoja binafsi zilikuwa zinakuja. Lakini pia hatukuwahi kushuhudia adhabu kwa wabunge wa upinzani kama ilivyokuwa kwa Bunge hili,” amesema Matiko.

“Bunge la 11 mwanzo tulianza kushuhudia askari wakiwa na sare wakiingia ndani kuwatoa wabunge wa upinzani. Zamani hakukuwa na askari wenye silaha lakini, imeshuhudiwa askari wenye sare na silaha wanaingia ndani,” amesema.

Hata hivyo, mara kadhaa Spika Ndugai alitoa ufafanuzi juu ya malalamiko yanayotolewa kuhusu bunge hilo akisema, wabunge walikuwa wanapewa adhabu nyingi, kutokana na kukithiri kwa vitendo vya utovu wa nidhamu.

Pia, Spika Ndugai alisema vikao vya Bunge hilo vilikuwa havirushwi mubashara kila mara, kutokana na wajumbe wake kadhaa kuwa na tabia ya kutoa lugha za ovyo na zisizo na staha.

Tarehe 16 Juni 2020, Rais John Magufuli akirihutubia kwa mara ya mwisho, alilipongeza Bunge la 11 chini ya Spika Ndugai jinsi lilivyoisaidia Serikali anayoiongoza kuwatumikia Watanzania.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

Chadema yamtaka Rais Samia aunde tume kuchunguza mauaji mgodi wa Barick

Spread the loveRAIS Dk. Samia Suluhu Hassan, ameombwa aunde tume huru kwa...

KimataifaTangulizi

Zuma akataliwa kugombea urais

Spread the love  TUME Huru ya Uchaguzi Afrika Kusini (IEC) imemwondoa rais...

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Nani anasema kuna hasara ATCL?

Spread the loveRIPOTI za makusanyo na matumizi ya fedha katika Kampuni ya...

Habari za SiasaTangulizi

CAG: Wastaafu, wenza wao chanzo NHIF kufilisika

Spread the loveRIPOTI ya ukaguzi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu...

error: Content is protected !!