July 7, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Escrow yarudi bungeni kwa kishindo

Mbunge wa Kigoma Mjini (CCM), Peter Serukamba akihojiwa na moja ya kituo cha radio hapa nchini

Spread the love

KASHFA ya uchotwaji fedha za Umma katika Akaunti ya Tegeta Escrow Sh. 306 bilioni, iliyofunguliwa kwenye Benki Kuu ya Tanzania (BoT) bado haijazimika, licha ya Serikali kujaribu kuwasafisha baadhi ya watuhumiwa ikidai hawahusiki. Anaandika Edson Kamukara … (endelea).

Mbunge wa Kigoma Mjini, Peter Serukamba (CCM) ndiye ameifufua bungeni akisema, kitendo hatua ya Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, kuwasafisha baadhi ya watuhumiwa wa kashfa hiyo ni ubaguzi na usanii usikubalika.

Wiki iliyopita, Ikulu ilitangaza kuwasafisha aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliachim Maswi na waziri wake, Prof. Sospeter Muhongo kwamba tume iliyoundwa kuchunguza tuhuma dhidi yao, haikuwakuta na hatia katika suala la miamala ya fedha za Escrow.

Pia, Ikulu kupitia kwa Balozi Sefue, iliwasafisha mawaziri watatu waliojiuzulu kwa shinikizo la Bunge katika kashfa ya oparesheni tokomeza, ikisema licha ya wananchi kupoteza maisha, kuteswa na mifugo kuuawa na askari waliotekeleza oparesheni hiyo, lakini viongozi hao hawakuhusika moja kwa moja.

Mawaziri hao ni Dk. Emmanuel Nchimbi (Mambo ya Ndani), Balozi Khamis Kagasheki (Maliasili na Utalii) na Dk. Mathayo David (Mifugo na Uvuvi).

Ikumbukwe kuwa sakata la escrow liliibuliwa bungeni na mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila (NCCR-Mageuzi) na baada ya ukaguzi wa Mdhibiti na Mkaguzi wa Fedha za Serikali (CAG) kufanyika, ilithibitika kwamba miamala hiyo ilifanyika kinyume cha sheria huku baadhi ya viongozi wakiwa wamenufaika na mgawo wa fedha hizo.

Akichangia hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi kwa ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka wa fedha 2015/16, katika eneo la utawala bora, Serukamba amesema “hii staili inayojaribu kutumika ni ya kizamani ya kusafisha watu kiani, imepitwa na wakati”.

Huku akisikilizwa na kushangiliwa na wabunge wengi, Serukamba amesema “kama Balozi Sefue anasema Maswi na mawaziri hao ni safi, basi atwambie Andrew Chenge (Bariadi Magharibi), Prof. Anna Tibaijuka (Muleba Kusini), William Ngeleja (Geita), uchafu wao ni upi wakati walipata mgawo halali?

Change, Ngeleja na Victor Mwambalaswa (Lupa), walivuliwa uenyekiti wa kamati za Bunge baada ya kuthibitika kuwa walipokea mgawo wa fedha hizo kutoka kwa mmoja wa wamiliki wa IPTL, James Rugemalira bila kutangaza maslahi kama sheria ya maadili ya viongozi wa umma inavyotaka.

Katika mtiririko huo, mawaziri Tibaijuka, Muhongo na aliyekuwa Mwanasheria Mkuu, Jaji Fredrick Werema walijiuzulu kutokana na kashfa hiyo huku baadhi ya watendaji katika mamlaka mbalimbali za serikali wakifikishwa mahakamani na kwenye Baraza la Sekretarieti ya Viongozi wa Umma.

Akizungumza kwa masikitiko kuhusu uamuzi huo wa Ikulu, Serukamba alishauri kuwa, “Chenge, Ngeleja, Werema, Mwambalaswa na mawaziri wengine waliowahi kujiuzulu kama sehemu ya uwajibikaji nao wasafishwe na kurudishwa katika nafasi zao.”

“Bunge hapa tuliomba ripoti ya oparesheni tokomeza lakini haijawahi kuletwa ila anajitokeza katibu mkuu kiongozi kusafisha baadhi ya watu. Huu ni usanii wa kuwasaidia watu wachache na kuumiza wengine kwa malengo binafsi. Hatuwezi kuwa na serikali yenye “double standards”.

“Lazima wakina Chenge, Tibaijuka na wengine wote mawaziri waliojiuzulu huko nyuma kwa kashfa ya Richmond nao waundiwe tume wasafishwe kama wakina Maswi, vinginevyo mna ajenda binafsi ya kujisafisha,” amesema.

Serukama ameongeza kuwa, wako watumishi wa Ikulu wenye tuhuma za escrow lakini bado wanaendelea kubaki kazini huku watumishi wengine wa umma katika taasisi zingine wakifikishwa mahakamani kwa jambo hilohilo na hivyo kuhoji hii ni serikali gani yenye ubaguzi wa aina hiyo?

“Kama ni kuunda Judicial Inquiry (Tume ya kimahakama), basi ifanyike kwa watuhumiwa wote. Hiki si Chama Cha Mapinduzi tunachokijua. Sasa kinachofuata hata hao mliowapeleka mahakamani kwa suala hilo watawashinda kutokana na uamuzi huu wa kusafisha baadhi ya watu.

“Katibu Mkuu Kiongozi anasema hiyo ripoti ya tokomeza hawezi kuileta bungeni badala yake anaisoma nusu nusu na kuwasafisha baadhi ya watu. Huu ni ubaguzi na labda tuambiwe kuna watu mnaowalenga lakini haitawezekana,” alisisitiza Serukamba na kushangiliwa.

error: Content is protected !!