October 22, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Escrow yamtaabisha Prof. Tibaijuka jimboni

Aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Prof. Anna Tibaijuka

Profesa Anna Kajumulo Tibaijuka, Mbunge wa Jimbo la Muleba Kusini akiwa kwenye Baraza la Sekretarieti ya Maadili ya Watumishi wa Umma mwaka jana

Spread the love

PROFESA Anna Tibaijuka-Mbunge wa Muleba Kusini (CCM), ameanza ziara jimboni inayotafsiriwa kama ya “kujitakasa” kutokana na kashfa ya mgawo wa sh. bilioni 1.6 za Akaunti ya Tegeta Escrow inayomkabili. Anaadika Edson Kamukara … (endelea).

Hatua hiyo inakuja baada ya mwanasiasa huyo kujaribu bila mafanikio kujitetea kwenye vyombo vya habari vya ndani na nje ya nchi ili asivuliwe wadhifa wake wa uwaziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

Prof. Tibaijuka amevuliwa uwazi pamoja na kusimamishwa kwa muda ujumbe wa Kamati Kuu ya CCM kwa kosa la kukiuka maadili ya viongozi wa utumishi wa umma akidaiwa kupokea sh. bilioni 1.6 kutoka kwa mmoja wa wabia wa Kampuni ya kufua umeme ya Independent Power Tanzania Ltd (IPTL), James Rugemalira.

Kwa mujibu wa vyanzo vyetu vya habari kutoka Muleba, Machi 13 mwaka huu, Prof. Tibaijuka alilazimika kuitisha kikao “kizito” nyumbani kwake ili kupata tathmini ya hali yake kisiasa jimboni baada ya kukumbwa na kashfa hiyo.

Katika kikao hicho kilichohudhuriwa na washirika wake wa karibu wakiwemo wanafamilia, viongozi wa CCM na wadau mbalimbali, inaelezwa kuwa mbunge huyo aliambiwa hali yake kisiasa jimboni ni tete tofauti na anavyofarijiwa na wasaidizi wake.

“Miongoni mwa waliomweleza ukweli ni mshirika wake wa karibu (anatajwa), huyu alimwambia namna ambavyo watendaji wake wameshindwa kuwa na mahusiano mema na wananchi na hivyo kumfanya achukiwe.

“Alichoshauriwa ni kuanza ziara ya haraka kutembelea kata zote huku akitekeleza ahadi alizotoa wakati wa kampeni za mwaka 2010 na vile vile kuendelea kutoa ahadi mpya ambazo zitatekelezwa iwapo atachaguliwa tena,”anaeleza mtoa taarifa.

Katika ziara hiyo ambayo imeanza Machi 15 mwaka huu, katika Kijiji cha Kiholele Kata ya Bureza, Prof. Tibaijuka anadaiwa kupata wakati mgumu wa kueleza jinsi alivyotekeleza ahadi zake, hali iliyomlazimu “kumwaga” fedha kutuliza upepo.

MwanaHALISIOnline imedokezwa kuwa mbunge huyo kabla ya kukumbwa na kashfa ya Escrow amekuwa akitoa michango ya maendeleo au kuhadi misiba kwa sh. 100,000 kupitia kwa wasaidizi wake lakini sasa anafanya hivyo mwenyewe tena kwa kuongea dau.

“Tangu sakata hili la Escrow ameongeza dau, anatoa sh. 150,000 kwa kila tukio na kazi hiyo imeanza juzi katika Kata ya Magata Karutanga kwenye msiba wa (anatajwa) na baada ya hapo alielekea katika msiba mwingine kata ya Karambi,”kinasema chanzo kingine.

Taarifa hizo zinaongeza kuwa akiwa katika Kata ya Gwanseli, Tibaijuka ambaye kwa siku nzima ya jana hakupatikana kufafanua madai hayo, anadaiwa kutoa sh. 250,000 kwa vijana aliowakuta wakicheza mpira kwenye kitongoji cha Kaina.

Akiwa Kata ya Bureza, Tibaiujuka alibanwa na wapiga kura aeleze kwanini hajatekeleza ahadi yake ya kuijenga barabara hiyo ambayo hata siku alipotembelea hapo alishindwa kufika kwa gari kutokana na kuharibiwa vibaya na mvua.

Kama alivyofanya kwenye maeneo mengine, pia Tibaijuka aliwaahidi wananchi hao kuwa atachangia sh. milioni 2 kwa ajili ya ukarabati wa barabara hiyo na kisha akatoa ada ya 100,000 kwa wanafunzi wawili (kila mmoja 50,000) na kuchangia sh. 100,000 kwa kikundi cha akina mama.

Kwa mujibu wa vyanzo vyetu, Prof. Tibaijuka alijikuta akilazimika kutengua ahadi yake ya kujenga kwa kiwango cha lami barabara kati ya Muleba hadi Hospitali Teule ya Wilaya ya Rubya yenye urefu wa km 13.  

Ahadi hiyo aliitoa mwaka juzi wakati wa ziara ya Rais Jakaya Kikwete, akisema kuwa serikali imekubali kuijinga barabara hiyo kwa kiwango cha lami kabla hajamaliza ubunge wake.

Lakini juzi alipobanwa na wapigakura wake, Prof. Tibaijuka amesema ahadi hiyo haitawezekana kutekelezeka kwa muda uliyobakia kwa vile hakujua kama kiasi cha fedha kinachohitajika zaidi ya sh. bilioni 21 kingekuwa kikubwa hivyo.

error: Content is protected !!