January 19, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Escrow kumuumbua Rais Kikwete

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete

Spread the love

RAIS Jakaya Mrisho Kikwete, anahaha kujiokoa na kashfa ya ukwapuaji wa mabilioni ya shilingi katika akaunti ya Escrow, ndani ya Benki Kuu (BoT).

Mpango wa sasa, ni kuwakamata baadhi ya waliopewa fedha na James Rugemalira, mmoja wa wamiliki wa IPTL ili kuzima mjadala. Saed Kubenea anaandika… (endelea).

Profesa Anna Tibaijuka, mbunge wa Muleba Kusini (CCM), yumo katika orodha ya wanaotakiwa kufikishwa mahakamani wakati wowote wiki hii.

Tayari Prof. Tibaijuka amehojiwa zaidi ya mara moja na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana Rushwa (TAKUKURU),  kuhusu Sh. 1.6 bilioni alizopewa na Rugemalira.

Mkakati wa kumfikisha mahakamani Prof. Tibaijuka, unasukwa kwa ustadi mkubwa na waziri mmoja mwandamizi katika serikali ya Rais Kikwete.

“Watanaka Prof. Tibaijuka apelekwe mahakamani kwa hoja kuwa, kwa hadhi aliyonayo kimataifa, sakata zima la Akaunti ya Tegeta Escrow litakuwa limezimwa,” anaeleza mtoa taarifa.

Anasema, “Lakini nataka nikuhakikishie, kitendo hicho kitasababisha tatizo kukua. Rais Kikwete anafahamu fika Harbinder Singh Sethi wa IPTL kuwa alitokea ikulu kabla ya kukwapua mabilioni ya shilingi kutoka akaunti ya Escrow.”

Anasema, “Ni vigumu kwa Rais Jakaya Kikwete kufanikiwa kujitenga na kashfa ya ukwapuaji wa zaidi ya Sh. 321 bilioni zilizochotwa katika akaunti ya Tegeta Escrow.”

Kiasi cha Sh. 321 bilioni zilikwapuliwa kutoka akanti ya Escrow ndani ya Benki Kuu (BoT), kati ya Septemba na Novemba 2013; na Prof. Tibaijuka alipewa Sh. 1.6 bilioni na mmoja wa waliokuwa wabia katika kampuni ya kufua umeme ya IPTL.

Taarifa zinasema, anayejiita na kuitwa na serikali kuwa ni “mmiliki mpya wa IPTL/PAP,” Harbinder Singh Sethi, aliletwa nchini na mmoja wa wanafamilia wa Rais Kikwete.

Taarifa zinasema, wanaoshinikiza Prof. Tibaijuka kufikishwa mahakamani wanajenga hoja mbili. Kwanza, kwamba hatua hiyo italegeza msimamo wa wahisani wa kuinyima misaada Tanzania; na kwamba kelele zote za ndani zitakuwa zimezimwa.

Pili, hatua ya kumfikisha mahakamani waziri huyo wa zamani wa ardhi, kutasaiidia kumkingia kifua waziri wa nishati na madini, Prof. Sospeter Muhongo na kuzima mjadala bungeni.

Rais Kikwete alimfuta kazi Prof. Tibaijuka katika mkutano wa “Wazee wa Dar es Salaam,” tarehe 23 Desemba 2014.

Inaelezwa kuwa singasinga alikutana na rais, ikulu jijini Dar es Salaam; na kutoka hapo alikwenda kukwapua mabilioni ya shilingi BoT hata bila kumfahamisha Rugemalira – mbia mwenzake.

Taarifa zinasema, sasa rais anashinikizwa kumfukuza  Prof. Tibaijuka kutoka Kamati Kuu (CC) ya CCM na baadaye kumfikisha mahakamani kwa madai ya wizi na utakatishaji wa fedha.

Kupatikana kwa taarifa kuwa serikali ya Rais Kikwete inapanga njama za wizi kwa kupeleka baadhi ya waliochotewa fedha na Rugemalira, kumekuja wiki tatu baada ya Kikwete kudai kuwa fedha katika akaunti ya Escrow, hazikuwa za umma.

Akihutubia wanaoitwa, “Wazee wa Dar es Salaam,” katika ukumbi wa Diamond Jubilee, Rais Kikwete alisema, mabilioni ya shilingi katika akaunti ya Escrow yalilipwa kwa PAP baada ya Mahakama Kuu kutoa “amri” tarehe 5 Septemba 2013.”

Akaunti ya Escrow ilifunguliwa ili kusubiri kumalizika kwa mgogoro kati ya Tanesco na IPTL, uliohusu madai ya udanganyifu katika uwekezaji; na hata gharama za kuweka mitambo – Capacity Charge – ambavyo vilifanywa na kampuni hiyo ya kigeni.

Kampuni ya IPTL ni muungano wa kampuni mbili – VIP Engineering and Marketing Limited ya James Rugemalira, iliyokuwa ikimiliki asilimia 30 ya hisa na MECHMAR ya Malaysia iliyokuwa na asilimia 70 za hisa.

error: Content is protected !!