May 6, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Elimu ‘yawagonganisha’ Jafo na Ndalichako

Spread the love

Suala la wizara ipi ina wajibu wa kusimamia uendeshwaji wa elimu hapa nchini limeendelea kugonga vichwa vya wabunge kama ambavyo limekuwa likizua mjadala kwa wachambuzi wa masuala ya elimu kwa muda sasa,anaandika Dany Tibason.

Swali la Mbunge wa Urambo, Magreth Sitta (CCM), limewafanya Selemani Jafo, Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), na Profesa Joyce Ndalichako wote kulazimika kutolea ufafanuzi suala hilo.

Sitta alihoji kuhusu mkanganyiko uliopo kwenye usimamizi wa sekta ya elimu ikiwemo usimamizi wa elimu ya kidato cha tano na sita kuwekwa chini ya Tamisemi kabla ya kurekebisha changamoto za elimu ya awali, msingi na sekondari.

“Suala la ubora wa elimu ni muhimu kusimamiwa na Wizara husika. Ni kwa nini wahusika wanakwepa jukumu lao na kulipeleka Tamisemi?” amehoji Mbunge huyo.

Akijibu swali hilo, Jafo amesema kwa kuzingatia matakwa ya Katiba na uendeshaji wake, ni wakati muafaka kwa elimu ya kidato cha tano na sita kuendelea kusimamiwa na Tamisemi.

“Ugatuaji wa madaraka ni suala la kikatiba kwa kuzingatia Ibara ya 145 na 146 ya Katiba ya Jamuhuri ya Muungano ya mwaka 1977 ambayo imetambua uwepo wa madhumuni ya Serikali za Mitaa kuwa ni kupeleka madaraka kwa wananchi.

Tumelenga kupeleka madaraka kwa wananchi ili kuwapa fursa ya kushiriki katika kuzisimamia na kuziendesha shule hizo,” amesema.

Katika hali iliyoonesha majibu ya Waziri Jafo kutoeleweka vyema, Profesa Joyce Ndalichako, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi naye aliomba kufafanua zaidi suala hilo.

Akitoa majibu ya nyongeza, Ndalichako amesema, “Wizara ya elimu pamoja na TAMISEMI tunafanya kazi kwa ukaribu sana, wao wana majukumu yao na sisi tuna yetu na pia yapo mambo tunayoshirikiana ikiwemo uboreshaji wa idara ya ukaguzi kwa shule kongwe.”

 

error: Content is protected !!