July 1, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Edward Moringe Sokoine: Jabali la kisiasa lisilosahaulika

Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere akiwa na marehemu Edward Moringe Sokoine

Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere akiwa na marehemu Edward Moringe Sokoine

Spread the love

MIAKA 31 iliyopita, taifa hili lilipoteza mmoja wa viongozi mahiri, shupavu, na kipenzi cha wanyonge, Edward Moringe Sokoine. Kifo chake kilikuwa pigo kubwa kwa kuwa alikuwa tayari amejitokeza na kujipambanua kama kiongozi mwenye uthubutu wa dhahiri katika kupigania na hata kufia maslahi ya raia, hasa maskini.

Kifo cha Sokoine hakikuwa cha kawaida. Hakikutarajiwa. Na kilitikisa taifa. Kilishtua wengi, kwani hakuwa ametoa kauli ya mwisho. Watu wengi, katika makundi mbalimbali – wakubwa kwa wadogo – waliomboleza huku wakitafakari juu ya hatma ya taifa, ikizingatiwa alifariki dunia akiwa waziri mkuu kipenzi cha Rais Julius Nyerere.

Waliokuwa wanafuatailia nyendo za kisiasa za kiongozi huyo, walihisi kuwa ndiye angekuwa mrithi wa Rais Nyerere. Sokoine alikuwa jemedari wa vita dhidi ya ulanguzi na uhujumu uchumi.

Wingu la simanzi lilitanda baada ya Redio Tanzania Dar es Salaam (RTD), kukatisha ghafla matangazo katika vipindi vyake mishale ya saa 11 jioni tarehe 12 Aprili 1984, na kuanza kupiga kwa mfululizo nyimbo za maombolezo.

Baada ya nyimbo hizo lilifuata tangazo rasmi la kifo hicho, likiwa ndiyo taarifa rasmi ya serikali kuhusu kifo cha Sokoine. Alifariki dunia katika ajali ya gari eneo la Dumila, Morogoro wakati anarejea Dar es Salaam akitokea bungeni Dodoma.

Huko bungeni aliwasha moto kabla ya kuondoka, hasa alipozungumza kuhusu  kubana matumizi ya serikali, ambako kuliambatana na hoja juu ya ukubwa wa serikali na hasa mantiki ya kuwa na mawaziri wasiokuwa na wizara maalum, lakini wakipatiwa haki zote sawa na mawaziri wenye wizara.

Sokoine alionyesha moyo wa kujitoa kuwatumikia wananchi mara tu baada ya kuteuliwa katika wadhifa wa waziri mkuu wakati huo akiwa mbunge wa Monduli mkoani Arusha. Katika utawala wake, kama waziri mkuu, aliendesha na kusimamia mwenyewe vita dhidi ya dhuluma iliyokuwa inaendeshwa na wachache wenye nacho dhidi  ya  wengi wasionacho.

Vita dhidi ya walanguzi na wahujumu uchumi ni miongoni mwa mambo ambayo yaliinua jina la Sokoine kila pembe ya nchi hii na katika medani za kisiasa.

Nyota yake ilizidi kung’ara na kuwa chachu ya kupendwa miongoni mwa walio wengi; akaonekana mwiba kwa walafi na wadokozi wa keki ya taifa. Kwa mfano, ni kiongozi aliyeleta mabadiliko dhahiri kwenye sekta ya usafiri.

Aliondoa ukiritimba wa makampuni kama UDA na KAMATA chini ya mwanvuli kile kilichoitwa ‘National Transport Corporation (NTC)’ kwa kuruhusu watu binafsi kusafirisha abiria. Ni kuanzia hapo makampuni kama UDA ambayo ndiyo pekee iliyokuwa na leseni ya kusafirisha abiria mkoani Dar es Salaam  na KAMATA iliyokuwa na leseni ya kusafirisha abiria wa mikoani yalianza kupata upinzani kutoka kwa wafanyabiashara binafsi wa mabasi ya abiria.

Ingawa kwa upande mmoja Sokoine alionyesha kupata mafanikio kwa kuungwa mkono na wananchi, kwa upande mwingine alijikuta akipoteza marafiki na kujijengea maadui lukuki kutokana na mfumo wa utendaji uliokuwepo kabla yake.

Katika utendaji wake mara zote, Sokoine aliamini katika siasa za uwazi. Alizungumza kile alichoamini ndicho na alisimamia na alionyesha mfano katika utekelezaji wa kila jambo alilotaka lifanyike.

Sokoine alipenda haki, aliona ni kitu cha kushangaza kwamba wananchi walio wengi walikuwa wanaishi maisha ya dhiki, hawakusikilizwa na watendaji. Alishangaa kuona kwamba urasimu umezama kwenye rushwa za nipe-nikupe na kuporomoka kwa maadili hasa upungufu mkubwa katika kutoa huduma na haki.

Sokoine alitumia uwezo kama waziri mkuu kujaribu kurejesha nidhamu katika sekta ya utawala kwa kuwajibisha viongozi na watendaji wabovu. Kwa upande mwingine, alijitahidi kuvunja ushirikiano kati ya viongozi warasimu na wafanyabiashara ambao kwa pamoja waligeuza sekta ya umma kama shamba la bibi.

Mambo mengi aliyojaribu kufanya Sokoine yalitokana na uthubutu wake binafsi. Alitumia mfano wake kama kiongozi ambaye alikuwa na uadilifu mkubwa na hakuwa na ubinafsi.

Rekodi ya utendaji kazi  wa kiongozi huyu ambaye alibahatika kushika wadhifa wa waziri mkuu katika vipindi viwili tofauti,  haijafikiwa na kiongozi yeyote katika ngazi hiyo, miongo mitatu tangu kifo chake. Inasemekana ni katika kipindi chake cha uongozi, Mwalimu Nyerere alipata ahueni, alinenepa.

Kifo cha Sokoine kilikuwa moja ya mapigo makuu aliyowahi kupata Mwalmu Nyerere akiwa rais, kwani alimtegemea mno katika kusimamia serikali. Alimwamini na alimuona kama “pacha wake” kwani wote wawili walisimamia kile walichoamini na walichoishi.

Viongozi wa aina ya Mwalimu Nyerere na Sokoine hawazaliwi kila mara. Si ajabu leo tusingekuwa tunazungumzia ombwe la uongozi kama Sokoine asingefariki ghafla, maana kama angekuwa rais baada ya Mwalimu Nyerere, yapo maeneo ambayo angeyasimamia kwa dhati, na kuacha urithi ambao ungekuwa wa msaada mkubwa kwa warithi wake.

Kifo chake kiliinyima Tanzania fursa hiyo. Kila awamu ya uongozi inapoingia madarakani inakuwa kama vile inaanza upya. Hakuna mwendelezo, hakuna urithi. Ndiyo maana tupo jinsi tulivyo leo. Na ndiyo maana Watanzania hawachoki kuwakumbuka Mwalimu Nyerere na Sokoine.

Kwa jinsi walivyoshibana kikazi, ni vigumu kukumbuka mmoja bila kukumbuka mwingine. Bahati mbaya wote wameshatangulia mbele ya haki. Mungu alaze roho zao mahali pema peponi!

Mwandishi wa makala hii ni Masumbuko Petro ambaye ni mwanafunzi-Chuo Kikuu Dar es Salaam. 0788-922230

error: Content is protected !!