November 29, 2021

Uhuru hauna Mipaka

DUWASA yaichapa 2-1 TangaUWASA

Spread the love

 

MAMLAKA ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mjini Dodoma (DUWASA), imeibuka kidedea kwa ushindi wa 2-1 ilioupata dhidi ya wapinzania wao Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Tanga (TangaUWASA). Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).

Imeibuka na ushindi huo mnono, leo Jumanne tarehe 9 Novemba 2021, ikicheza kandanda safi na la kuvutia katika michuano ya fainali za ligi ya Maji Cup 2021 hatua ya makundi inayofanyika viwanja vya Social UDOM jijini Dodoma.

Licha ya kusakata kandanda lenye kuvutia na kuamsha shangwe kwa mashabiki waliokuwa wakifuatilia kandanda hilo, DUWASA iliwalazimu kusubiri hadi dakika za jioni kujihakikishia ushindi huo.

DUWASA walikuwa wa kwanza kufumania nyavu za TangaUWASA, dakika za mwanzo tu za mchezo huo kwa John Julius kuifungia mamlaka hiyo, ya makao makuu ya nchi, Dodoma.

Hadi timu hizo zinakwenda mapumziko, DUWASA ilikuwa kifua mbele kwa 1-0. Hata hivyo, kipindi cha pili kilianza kwa kasi kwa timu zote kushambuliana kwa zamu na
TangaUWASA ilijikuta ikipata penati ambayo waliitumia vyema kusawazima.

Hata hivyo, DUWASA inayonolewa na kocha wake matata, Khalifa Ismail, iliendelea kulisakama lango la TangaUWASA na kufanikiwa kujipatia goli la pili na la ushindi dakila za mwisho za mchezo huo.

Mara baada ya mchezo huo kumalizika, Ismail amesema, mchezo huo ulikuwa mzuri na wenye ushindani mkali lakini vijana wake, aliokuwa amewaandaa vyema hawakumuangusha.

“Matokeo haya ni kutokana na kuiandaa vizuri timu na kuwapa motisha wachezaji kwamba sisi ndio mabingwa na kama ni mabingwa lazima tucheze kibingwa na hiki ndicho kimetokea,” amesema Khalifa

DUWASA itaingia tena uwanjani kusaka pointi tatu muhimu kesho jioni dhidi ya timu ya Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Kahama (KUWASA), mkoa wa Shinyanga.

Mashindano ya Maji Cup yalizinduliwa tarehe 6 Novemba 2021 kwa ufunguzi wa mechi kati ya DUWASA na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mbeya (Mbeya UWSA) ambapo DUWASA ilipoteza mchezo wake kwa kupigwa goli tatu.

Mashindano hayo yanayoendelea katika jijini Dodoma kwa kushirikisha timu za Mamlaka ya Maji kutoka sehemu mbalimbali nchini ikiwa yanalengo ya kuhamasisha mapambano dhidi ya upotevu wa Maji.

error: Content is protected !!