VIONGOZI wa kimataifa wameungana na Watanzania kuomboleza kifo cha Rais wa Tanzania, Dk. John Magufuli. Anaripoti Hamis Mguta, Dar es Salaam…(endelea).
Rais Magufuli alifariki dunia jana tarehe 17 Machi 2021, saa 12.00 jioni katika Hospitali ya Mzena, jijini Dar es Salaam, alikokuwa anapatiwa matibabu kutokana na maradhi ya moyo.
Waziri Mkuu wa Uingereza, Boris Johnson, amesema amesikitishwa na kifo cha Rais John Magufuli.
“Nimesikitika kusikia kwamba Rais wa Tanzania, John Magufuli ameaga dunia, mawazo yangu yako kwa wapendwa wake na watu wa Tanzania.
Katika kuomboleza kifo hicho, Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta ametangaza siku saba za maombolezo kuanzia leo.
“Nimepoteza rafiki nimepoteza kiongozi mwenzangu na Kenya tunasimama na wenzetu wa Tanzania katika wakati huu mgumu,” amesema Rais Kenyatta.

Rais wa Somalia, Mohamed Farmaajo naye pia ametuma salamu za rambirambi.
“Kwa niaba yangu na kwa niaba ya serikali ya Taifa la Somalia ningependa kuwasilisha rambirambi zetu kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kumpoteza kiongozi Rais Magufuli, tunalitakia taifa zima na serikali subra na utulivu katika kipindi hiki cha maombolezo,” amesema Rais Farmaajo.
Rais wa Uganda, Yoweri Museveni kupitia ukurasa wake wa Twitter, amesema Rais Magufuli alikuwa kijana bora wa Afrika, kufuatia msimamo wake wa kuwakomboa kiuchumi Waafrika hasa wa Afrika Mashariki.
“Kwa masikitiko makubwa nimepokea kifo cha Mheshimiwa Rais Mgaufuli, alikuwa kiongozi mzuri anayeamini na kusimamia uwezeshaji wa kiuchumi kwa watu wa Afrika Mashariki.
“Tunaungana na Watanzania kuomboleza kifo cha kijana bora wa Afrika. Roho yake upumzike kwa amani,” amesema Rais Museveni.

Lazarus Chakwera, Rais wa Malawi amesema, Rais Magufuli alikuwa alama kubwa ya ufufuo wa uchumi wa Afrika na kwamba kuondoka kwake ni pigo kwa bara hilo.
“Nimepokea kwa mshtuko na masikitiko kifo cha rafiki na kaka yangu Magufuli, natuma salamu zangu za pole kwa familia ya Rais Magufuli na Watanzania kwa ujumla. Rais Magufuli alikuwa ishara kubwa ya ufufuo wa uchumi wa Afrika na kufa kwake ni hasara kwa bara hili,” amesema Chakwera.
Rais wa Namibia, Hage Geingob katika mtandao wake wa Twitter ameandika “Tanzania imepoteza mzalendo, Namibia imepoteza kaka, Namibia inaungana na watu wa Tanzania kuomboleza kifo cha kaka yetu mpendwa, Rais Magufuli. Katika kipindi hiki cha maombolezo natuma salamu zangu za pole kwa familia na watu wa Tanzania.”
Balozi wa Marekani nchini Tanzania, Donald J. Wright amesema, Marekani inasimama na Watanzania katika kipindi hiki kigumu.
“Kwa niaba ya watu wa Marekani nitatoa salamu zangu z arambirambi katika maombolezo ya kifo cha Rais Magufuli, Mtambue kwamba Marekani inasimama na Watanzania katika kipindi hiki kiigumu,” amesema Balozi Wright.
Leave a comment