January 19, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Duni: Katiba ya ‘Warioba’ ndio itaondoa ufisadi

Spread the love

MGOMBEA Mwenza wa urais kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) anayewakilisha Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), Juma Duni Haji, amesema umoja huo umejiamini utatekeleza ahadi wanazozitoa kwa kuwa usimamizi utakuwa chini ya Katiba itakayotokana na rasimu iliyoandaliwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba. Anaandika Pendo Omary … (endelea).

Duni ametoa kauli hiyo jana alipohutubia mkutano wa kampeni jimbo la Ubungo, Dar es Salaam uliofanyika Mburahati. Katika mkutano huo ulioandaliwa na timu ya kampeni ya mgombea ubunge wa Ubungo, Duni alimuombea kura mgombea urais wa Tanzania kupitia UKAWA, Edward Lowassa.

Katika mkutano huo pia mgombea ubunge, Saed Kubenea alihutubia pamoja na mgombea udiwani wa Kata ya Mburahati, Hemed Ally Sabula, mgombea udiwani wa kata hiyo.

Duni ambaye alikuja Dar es Salaam akitokea mkoani Tabora, amesema iwapo wananchi watawachagua wagombea wa chama hicho pamoja na waliosimamishwa na vyama vinavyoshirikiana katika muungano wa UKAWA, watarudi kuitumia rasimu ya Tume iliyoongozwa na Jaji mstaafu Joseph Warioba kupata katiba inayoridhiwa na wananchi.

Amesema chini ya Katiba yenye misingi ya kuwawajibisha viongozi wabovu na wabadhirifu, serikali ya UKAWA itakuwa na uhakika wa kutekeleza kwa mafanikio sera na ahadi zinazotolewa kipindi cha kampeni.

Duni amesema hali hiyo ni tofauti na wanavyofanya kimazoea viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kutoa ahadi ambazo hazikutekelezeka kutokana na wenyewe kutoogopa ufisadi.

Akizungumzia maendeleo ya halmashauri, Duni alisema serikali ya UKAWA itasimamia halmashauri za jijini Dar es Salaam, na kupitia upya mpango wa maendeleo ya jiji kwa lengo la kujenga makazi ya kisasa kazi itakayofuatana na ujenzi wa miundombinu imara kama vile barabara.

Amesema lengo hilo linakusudiwa kusaidia wakazi kuondokana na mazingira mabaya ya uchafu yanayozidi wakati wa mafuriko kama inavyoshuhudiwa mara nyingi zinaponyesha mvua kubwa.

“Iwapo mtatuchagua, katika jiji la Dar es Salaam tutahakikisha wananchi wanapata maji, jiji linakuwa na mitaro ya kupitisha majitaka, upatikanaji wa uhakika wa umeme na kuimarisha afya, elimu na shughuli za utamaduni.

“Tutatoa elimu kuanzia darasa la kwanza hadi chuo kikuu kwa watoto wote kwa gharama za serikali. Hii ni haki yenu sio fursa. Hadi leo usafiri Dar es Salaam ni mbaya. Shida hii ni lazima iondoke mkitupa ridhaa kuunda serikali. Siasa maana yake ni kushughulika na matatizo ya wananchi na kubadilisha mabaya katika uzuri.

“Ili tuweze kuyafanya hayo, lazima tupate Katiba ya wananchi sio Katiba ya CCM. Katiba Inayopendekezwa ambayo waliipitisha wajumbe waliopumbazwa na CCM haiwezi kutufikisha huko,” amesema.

Katiba iliyopitishwa na Bunge Maalum la Katiba imefuta Ibara 124(1)(b) inayowapa haki wapigakura kumwajibisha mbunge wao endapo wataona ameshindwa kuwasilisha au kutetea kwa dhati mambo yenye maslahi nao katika jimbo.

error: Content is protected !!