January 25, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Duni Haji: Tutarejesha Katiba ya Wananchi

Spread the love

MGOMBEA mwenza wa urais kupitia Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), Juma Duni Haji ameahidi Watanzania kuwa serikali itakayoundwa na kundi hilo baada ya kushinda uchaguzi mkuu itasimamia kurudishwa kwa Katiba ya Wananchi. Anaandika Pendo Omary … (endelea).

Duni ambaye atakuwa Makamu wa Rais katika serikali hiyo mpya, akimsaidia mgombea urais Edward Lowassa, amesema, “Iwapo mtatuchagua, tutahakikisha tunaleta Katiba iliyokubaliwa na wananchi, ambayo kwa miaka zaidi ya 50 ya uhuru hatujawahi kuipata.”

Duni alitoa ahadi hiyo leo katika hotuba yake kwenye mkutano wa uzinduzi wa kampeni ya UKAWA, umoja unaoundwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Chama cha Wananchi (CUF), National League for Democracy (NLD) na NCCR-Mageuzi.

Kwa sababu sheria ya Tanzania hairuhusu vyama vya siasa kuungana, UKAWA wamekubaliana kusimamisha mgombea wa pamoja akiwakilisha Chadema, kilichoafikiwa kutoa mgombea.

Duni alijiunga naye baada ya kuhama CUF, kilichopewa nafasi ya kutoa mgombea mwenza. Akiwa CUF, Duni ambaye ni mtaalamu wa takwimu na utawala wa fedha, alikuwa Makamu Mwenyekiti wa CUF na kulazimika kujiuzulu ili kushika nafasi hiyo.

Ukawa ingawa walishaanza kufanya kampeni kwa staili ya kukutana na makundi mbalimbali ya wananchi, kama vile kupanda daladala na kukagua masoko ya Tandale, Tandika kabla ya kuzuiwa alipokuwa anawasili Soko Kuu la Kariakoo, ndio imezindua rasmi kampeni zake kwenye viwanja vya Jangwani, Dar es Salaam.

Huku akishangiliwa kwa nguvu na umma uliofika kushuhudia uzinduzi huo, Duni alisema serikali itakayoongozwa na UKAWA, itaunda Tume ya Maridhiano, hatua ya kuwezesha ujenzi wa nchi kwa amani na maelewano ambapo watu watatakiwa kusameheana kwa kufuta yaliyopita na kuangalia mbele.

“Kwa sababu ya kuonewa na kukosa haki, mkituchagua tutaunda Tume ya Maridhiano ili tusameheane, tujenge nchi vinginevyo kutakuwa na uhasama,” amesema Duni.

Amesema serikali itasimamia huduma bora za jamii kama vile afya ikitilia mkazo uzazi salama kwa lengo la kupunguza vifo vinavyotokana na uzazi na kujenga heshima kwa wanawake aliosema ndio waathirika wakubwa wa huduma duni za afya nchini.

“Tutawaheshimu akina mama. Wanawake ndio walezi. Hawapewi likizo wala kiinua mgongo kwa kuzaa watoto 10. Tunaahidi tutawaheshimu wanawake kwa kuhakikisha wanapata huduma bora za afya na lishe kwa watoto,” amesema.

Akihutubia umma, Mwenyekiti wa BAWACHA, Halim Mdee amesema

Katika tukio lisilotarajiwa mapema, muongoza mkutano huo, John Mrema, ambaye ni Mkurugenzi wa Bunge wa Chadema, alimpandisha jukwaani Richard Tambwe Hiza aliyekuwa Afisa wa Kitengo cha Propaganda cha Chama Cha Mapinduzi (CCM) aliyehama CUF miaka kadhaa iliyopita.

Tambwe ambaye akiwa CUF alikuwa Mkurugenzi wa Habari na Uenezi, na mwanasiasa shupavu aliyeweka historia mbaya ya kuligawa jimbo la Temeke wakati akiaminika alishinda uchaguzi wa 2000, amesema wapo watu wengi ndani ya CCM wanapenda mabadiliko lakini wanaogopa kutoka na hivyo kuchelewesha upatikanaji wa mabadiliko.

“Tukiwa tunaogopa maneno, hatuwezi kuleta mabadiliko. Namshangaa Mwakyembe kwa maneno yake mwenyewe aliniambia atapinga mpaka mwisho uuzwaji wa Benki ya Taifa ya Biashara (NBC). Wakati huo Mwakyembe akiwa Mjumbe wa Bodi ya benki hiyo. Halafu leo anatumika kumchafua Lowassa,” alisema.

Tambwe alimtaja Dk. Harisson Mwakyembe wa CCM katika hilo akimshangaa maneno aliyosema ya ovyo aliyoyasema katika kumnadi mgombea urais wa CCM, Dk. John Magufuli mjini Kyela, ambako naye anatetea kiti cha ubunge.

Kabla ya hotuba za wagombea kuanza, ilikuwa zamu ya Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe kuizindua Ilani ya Uchaguzi (Manifesto) itakayopigiwa kampeni na wagombea hao pamoja na wale wanaowania ubunge na udiwani kupitia vyama vya UKAWA.

Pia Mbowe aliwaita wagombea ubunge wa majimbo ya Dar es Salaam, ambapo alisema kwa majimbo ya Segerea na Kigamboni wapo wagombea wawili-wawili mpaka keshokutwa yatakapofikiwa maamuzi ya kupatikana mgombea mmoja kila jimbo.

Katika majimbo hayo, CUF imemteua Julius Mtatiro kugombea Segerea wakati Chadema imemteua Anatropia Theonest. Kwa jimbo la Kigamboni, CUF imemteua Juma Shabani Mkumbi.

Wagombea wa majimbo mengine ni Saed Kubenea (Chadema, Ubungo), Kondo Bungo (CUF, Mbagala), Maulid Said (Kinondoni, CUF), Halima Mdee (Kawe, Chadema), Abdallah Mtolea (Temeke, CUF), John Mnyika (Kibamba, Chadema), Mwita Waitara (Ukonga, Chadema) na Muslim Hassanali (Ilala, Chadema).

error: Content is protected !!