January 23, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Duni: Chagueni Ukawa msile mavi Dar

Spread the love

MGOMBEA Mwenza wa urais kupitia Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) kwa tiketi ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Juma Duni Haji, amesema iwapo wananchi watamchagua Edward Lowassa watajipa uhakika wa kuondokana na tatizo sugu la maji. Anaandika Pendo Omary … (endelea).

Duni ametoa ahadi hiyo leo wakati wa ziara ya kampeni jimboni Segerea jijini Dar es Salaam alikohutubia na kuondoka kwenda Zanzibar kuungana na mgombea urais wa Zanzibar kupitia CUF, Maalim Seif Shariff Hamad aliyezindua kampeni leo.

Duni alitakiwa kufanya ziara katika majimbo mengine ya Temeke na kigamboni lakini akashidwa kutokana na kuhitajika katika mkutano wa kufungua kampeni za Serif visiwani Zanzibar.

Hivyo mikutano hiyo kuendeshwa na viongozi na makada wa vyama vya Ukawa wakiwemo Makamo Mwenyekiti (Chadema) Zanzibar, Said Issa Mohammed, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake wa CUF Wilaya ya Kinondoni, Blandina Masabwite, aliyekuwa mbunge wa jimbo la Mkanyageni, Pemba, Mohamed Mnyaa na Suzan Lyimo wa Chadema.

Amesema “Leo jua kali watu wanaugua kipindupindu jijini Dar es Salaam. Ni kwa sababu wanakunywa mavi (maji yaliyochanganyika na kinyesi). Tutahakikisha jijini la Dar es Salaam watu hawanywi mavi. Tatizo la maji litakwisha. Tutashirikiana na halmashauri,” amesema Duni.

Ameahidi kuwa serikali itakayotokana na Ukawa itasimamia huduma za afya na elimu kutolewa kwa ufanisi, pamoja na kupunguza kodi kwa lengo la kuvutia ulipaji wa hiyari na kuhakikisha jiji linaondokana na uchafu.

“Tukiingia madarakani matibabu ya mama na mtoto yatakuwa chini ya gharama za serikali, kupitia mpango wa bima,” amesema Duni.

Aidha, amesema “watoto wa masikini watasoma bila Malipo kuanzia darasa la kwanza mpaka watakaposhidwa wenyewe,” amesema Duni.

Mgombea ubunge jimbo la Segerea anayewakilisha Ukawa, Julius Mtatiro (CUF) amesema akichaguliwa kuwa mbunge atashirikiana na wananchi kuimarisha miundombinu ya barabara na kusimamia huduma bora za afya, maji na kuanzisha mifuko ya kuweka na kukopa ngazi ya Kata.

“Baada ya taarehe 25 Oktoba nitahakikisha mbunge wenu anakuwa na ofisi hapahapa Segerea. Nitaanzisha mifuko ya kata ya kuweka na kukopa ya vijana na akinamama,” amesema Mtatiro. Jimbo hilo halina ofisi ya mbunge.

Blandina amesema wanawake na watoto watafurahi kupata serikali inayowaangalia kwa kuwa hali zao ziko hoi. “Tunataka serikali itakayolinda maslahi yetu mama na watoto…. itakayoleta ajira kwa vijana.”

error: Content is protected !!