WACHUNGUZI kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wamesema wanao ushahidi wa kutosha unaoonyesha hatua kwa hatua namna maadui wanavyotaka kuiyumbisha nchi hiyo. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea)
Katika taarifa iliyosomwa kwenye televisheni ya taifa jana tarehe 8 Februari, 2022 na Msemaji wa Rais Felix Tshisekedi, Tharcisse Mwema amesema jaribio hilo linalolenga kuvuruga taasisi za kidemokrasia halitavumiliwa.
Taarifa hiyo imetolewa siku chache baada ya François Beya ambaye ni mshauri maalum wa usalama wa Rais Tshisekedi kukatamwa tarehe 5 Februari mwaka huu.
Tukio hilo lilitokea wakati rais huyo alipokuwa akihudhuria mkutano wa kilele wa Umoja wa Afrika katika mji mkuu wa Ethiopia, Addis Ababa.
Kukamatwa kwa kigogo huyo kulizua maandamano, huku wanachama wa chama cha rais wakiingia mitaani.
Aidha, Msemaji huyo wa rais amesema uchunguzi unaendelea na hali imedhibitiwa.
Pamoja na mambo mengine imeelezwa kuwa ukimywa wa serikali na ofisi ya rais tangu kisa hicho cha Jumamosi kutokea, kimechochea tetesi za ukosefu wa utulivu nchini.
Hadi sasa Beya na hata mawakili wake hawajatoa taarifa yoyote kwa umma kuhusiana na kukamatwa kwake.
Leave a comment