July 28, 2021

Uhuru hauna Mipaka

DPP kumsulubu ‘TISS’ wa UVCCM Arusha

Spread the love

SAKATA la Lengai Ole Sabaya, Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM), Mkoa wa Arusha, kutuhumiwa kujihusisha na vitendo vya wizi na utapeli akitumia kitambulisho cha Idara ya Usalama wa Taifa (TISS), lipo mikononi mwa mwendesha mashitaka wa Serikali (DPP), anaandika Charles William.

Sabaya amekuwa akituhumiwa kujihusisha na vitendo vya utapeli mkoani Arusha kwa muda sasa huku Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha likidaiwa kumlinda na kutomfikisha mahakamani kila anapofungiliwa mashitaka na watu mbalimbali.

Tuhuma dhidi ya Sabaya zimekuwa zikitolewa sambamba na kuwekwa wazi kwa picha za vitambulisho ‘feki’ vya Idara ya Usalama wa Taifa ambavyo kijana huyo anadaiwa kuvitumia katika utapeli huo.

Charles Mkumbo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha ameiambia MwanaHALISI online kwa njia ya simu kuwa, Jeshi la Polisi mkoani Arusha halimkingii kifua mtuhumiwa huyo, bali linasubiri ruhusa ya DPP ili kuandaa mashitaka yake ndipo limfikishe mahakamani.

“Hakuna kesi iliyozimwa, malalamiko yote yaliyofikishwa polisi yanachunguzwa na kufikishwa kwa Mwanasheria wa Serikali kwaajili ya kuandaa mashitaka ili aweze kufikishwa nmahakamani,” amesema Kamanda Mkumbo.

Wakati RPC huyo akisema hayo, hapo awali, Sabaya ambaye pia ni diwani wa kata ya Samabashi wilaya ya Arumeru, mkoani Arusha aliiambia MwanaHALISI online, tuhuma hizo zinatolewa na watu wanaofanya kazi ya Ibilisi.

“Wanaonituhumu wanafanya kazi kwenye karakana ya Ibilisi, hivi karibuni ngano na magugu vitatengwa. Mimi sitoacha kupambana na rushwa za kihalifu ndani ya miradi ya UVCCM Mkoa na viongozi wote waliohusika na hili lazima wawajibishwe,” amesema Sabaya.

Hata hivyo, Sabaya hakuwa tayari kufafanua kuhusu kitambulisho cha Idara ya Usalama wa taifa kinachodaiwa kuwa chake, hakutaka pia kufafanua kiundani kuhusu watu mbalimbali kumshitaki kwa utapeli katika kesi  zilizo vituo mbalimbali vya polisi mkoani Arusha.

Miongoni mwa utapeli anaodaiwa kuufanya Sabaya ni pamoja na kulala na kula katika hoteli mkoani Arusha huku akigoma kulipia gharama kwa madai kuwa yeye ni mtumishi wa TISS lakini pia kuchukua fedha kwa watu, akiahidi kuwatafutia kazi kwani yeye ni ofisa usalama wa taifa.

Juzi (Alhamis) baadhi ya vijana wa UVCCM mkoani Arusha, walitwangana makonde wakati baadhi yao walipotaka kufunga minyororo na kufuli katika ofisi za umoja huo ili kumzuia Sabaya kuingia ofisini hapo kwa madai kuwa hana maadili ya kuendelea kuwa kiongozi.

Suala hilo lilisababisha Shaka Hamdu, Kaimu Katibu wa UVCCM kusafiri mpaka mkoani hapo ili kusuluhisha mgogoro huo huku akilitaka jeshi la polisi lichunguze na kuchukua hatua dhidi viongozi wa UVCCM wanaotuhumiwa kwa makosa ya jinai.

 

error: Content is protected !!