May 29, 2022

Uhuru hauna Mipaka

DPP azungumza na Masheikh wa uamsho

Spread the love

 

MKURUGENZI wa Mashtaka nchini (DPP), Sylvester Mwakitalu, amefanya mazungumzo na Masheikh wanaokabiliwa na tuhuama za ugaidi, ikiwemo Viongozi wa Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu Zanzibar. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam…(endelea).

Taarifa hiyo ilitolewa jana Jumanne, tarehe 15 Juni 2021 na Ibrahim Mkondo, Msemaji wa Shuraa ya Maimamu Tanzania, akielezea ziara ya Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu, Sheikh Issa Ponda, ya kuwatembelea masheikh hao katika Gereza la Ukonga, jijini Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa taarifa ya Mkondo, DPP Mwakitalu alifanya mazungumzo na Masheikh hao Jumamosi ya tarehe 12 Juni mwaka huu. Mazungumzo hayo yalichukua muda wa saa mbili na nusu.

“Masheikh walimueleza Sheikh Ponda kuwa, DPP alifika gerezani hapo siku ya Jumamosi, majira ya saa nne asubuhi na kufanya maongezi nao yaliyodumu kwa takriban masaa mawili na nusu,” ilisema taarifa ya Mkondo.

Taarifa ya Mkondo ilisema kuwa, DPP Mwakitalu alipokea changamoto za Masheikh hao, pamoja na wale walioko katika mahabusu za mikoani, wanaotuhumiwa kwa makosa mbalimbali.

“Masheikh hao hasa wale wenye kesi ambazo hazijaanza kusikilizwa, wamesema ziara hiyo imefufua matumaini yao ya kuanza kusikilizwa kesi zao, ambazo kwa zaidi ya miaka minane hazijaanza kusikilizwa kwa madai ya kutokamilika upelelezi,’ ilisema taarifa ya Mkondo.

Kwa mujibu wa taarifa ya Mkondo, Sheikh Ponda ametoa wito kwa Ofisi ya DPP kuharakisha usikilizwaji wa kesi, zilizokwama kwa sababu mbalimbali.

“Sheikh Ponda amemtaka Mkurugenzi huyo mpya kuhakikisha kesi za ugaidi zilizowajaza Waislamu magerezani katika mikoa mingi, zinaanza kusikilizwa.

Amesema sera ya kukaa na mashauri bila ya kuzungumzwa na kuwarundika watu magerezani kwa hoja ya kutafuta ushahidi, aiondoe ofisini kwake ili kumsaidia Rais Samia Suluhu Hassan, kulipeleka Taifa katika utawala wa haki na ubinadamu,” imesema taarifa ya Mkondo.

Masheikh wa Uamsho takribani 51 wanasota rumande kwa zaidi ya miaka nane, tangu walipokamatwa katika nyakati tofauti 2012.

Masheikh hao wanakabiliwa na Kesi ya Jinai Na. 121/2021, katika Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam.

Watuhumiwa hao wanadaiwa kati ya Januari 2013 na Juni 2014, walijihusisha na makosa ya ugaidi, kinyume na kifungu cha 27 (c), cha Sheria ya Kuzuia Ugaidi ya mwaka 2002.

error: Content is protected !!