November 27, 2022

Uhuru hauna Mipaka

DPP akoleza moto ‘Mbowe anataka nimfunge?’

Biswalo Mganga, aliyekuwa Mkurugenzi wa Mashtaka Tanzania (DPP)

Spread the love

BISWALO Mganga, Mkurugenzi wa Mashtaka nchini Tanzania (DPP) amehoji, ‘Mbowe (Freeman Mbowe) anataka nimfunge?’ Anaripoti Mwandishi Wetu, Moshi … (endelea).

Ametoa kauli hiyo leo tarehe 2 Desemba 2020, Moshi mkoani Kilimanjaro wakati akitoa taarifa ya kuwafutia mashtaka watuhumiwa 72, waliokidhi sifa kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kubambikiwa kesi.

DPP Mganga amesema, yeye ndiye aliyemfutia mashitaka Nusrat Hanje, aliyekuwa katibu mkuu wa baraza la vijana la Chadema (Bavicha) na wenzake.

Nusrat na wenzake, walikuwa na kesi mkoani Singida na tarehe 23 Novemba 2020, DPP aliwafutia mashtaka.

Amesema, kuna baadhi ya watu akiwemo Mbowe, Mwenyekiti wa Chadema Taifa, wakihoji namna Nusrat alivyotoka mahabusu na kwenda Dodoma kuapishwa kuwa mbunge wa viti maalum jijini Dodoma tarehe 24 Novemba 2020 wakati taarifa zake zikieleza anashikiliwa.

Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chadema

Sintofahamu ya Nustar iliyoibuka ndani ya Chadema baada ya wanachama wake 19, wakiongozwa na Halima Mdee, aliyekuwa Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake la chama hicho (Bawacha), kuapishwa kuwa wabumge wa viti maalum.

Mdee, Nusrat na wenzake wanatuhumiwa kusaliti msimamo wa Chadema wa kutotaumbua matokeo ya uchaguzi mkuu uliofanyika tarehe 28 Oktoba 2020, kwa kujipeleka kuapishwa kinyume na Katiba ya chama hicho.

Chadema walihoji kitendo cha Nusrat kutoka mahabusu moja kwa moja na kwenda Dodoma kuapishwa licha ya kutojaza fomu za kuomba kugombea nafasi hiyo, wakati alitoka mahabusu ikiwa muda wa kujaza fomu hizo umepita.

“Mnasema kuna mwanachama ameachiwa nje ya utaratibu, kesi nimefuta mimi DPP kwa mamlaka niliyonayo kisheria chini ya kifungu cha 91 kisheria cha mwenendo wa makosa ya jinai.”

Nusrat Hanje, Aliyekuwa Katibu wa BAVICHA

“Na wale walikuwa na kesi gani? wameenda kufanya mkutano, wakaimba wimbo wa Taifa, wakaongeza maneno Mungu Ibariki Chadema,” amesema Biswalo na kuongeza:

“Ni kinyume na taratibu, sasa wanaolalamika nimefuta kinyume na utaratibu, mmoja wapo ni Mbowe. Mbowe na wenzake siku wanachaguana viongozi nani awe mgombea Mliman City, waliimba wimbo wa Taifa wakaongezea maneno Mungu Ibariki Chadema, si waliimba?

“ …sasa mnataka nifanye kazi kwa upendeleao? au na yeye na wenzake anataka nimkamate nimpeleke gerezani kama hawa nilivyowapeleka?”

Amesema, hakumchukulia hatua Mbowe kwa kuwa, ilikuwa wakati wa kuelekea uchaguzi mkuu na kwa maslahi ya Taifa alilazimika kumwacha ili kuepusha migogoro.

“Kama ilifika hatua nikasema kwa maslahi ya Taifa, nikasema hawa nisiwapeleke maana tungeanza kuvurugana na uchaguzi na vitu vingine, nikasema basi ngoja niwaache. Kwanini wanataka hawa ndio niendelee, niwaweke ndani wakati wamefanya kosa la aina moja?

“Kama wanataka na wao niwapeleke kwasababu jinai haiozi, hakuna kinachonizuia DPP leo kumfungulia Mbowe na wenzake, kuwafungulia hata hawa niliowaachia kuwarudisha gerezani kwa kesi ile ile,” amesema.

Nusrat ambaye alikuwa Katibu wa Baraza la Vijana Chadema (Bavicha), alikaa mahabusu siku 133, jina lake lilikuwa miongoni mwa majina 19 ya wanawake walioapishwa tarehe 24 Novemba 2020, jijini Dodoma kuwa wabunge wa viti maalum.

DPP Mganga amesema “sasa wasitafute vitu vingine ambavyo havistahili, sheria ipo na inaruhusu, hakuna sheria inayosema mfungwa atolewe saa ngapi.”

error: Content is protected !!