Wednesday , 8 February 2023
Home Gazeti Habari Mchanganyiko DPP afuta kesi ya Lissu na wenzake
Habari MchanganyikoTangulizi

DPP afuta kesi ya Lissu na wenzake

Spread the love

 

KESI ya jinai Namb. 208/2016 iliyohusu mashitaka ya uchochezi dhidi ya Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Bara, Tundu Lissu, na wenzake watatu wakiwemo Wahariri wa gazeti la MAWIO, imefutwa. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, imefuta mashtaka dhidi ya Lissu, Wahariri Jabir Idrissa na Simon Mkina wa gazeti la MAWIO, na Ismail Mehboob aliyekuwa meneja wa kiwanda cha uchapishaji magazeti cha Flint.

Baaada ya Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP), kuiambia mahakama leo Jumatano, tarehe 22 Septemba 2021, kuwa Serikali haina tena nia ya kuendelea na mashtaka yote matano, dhidi ya washitakiwa hao.

Wakili wa Serikali, Ashura Mzava akimwakilisha DPP, baada ya utambulisho wake na mawakili wenzake wa upande wa utetezi, mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi Joseph Luambano, aliiambia Mahakama kuwa Serikali haina tena nia ya kuendelea na mashitaka yanayowakabili washitakiwa hao.

Wakili Mzava alisema DPP, Sylvester Mwakitalu, ameamua kuchukua hatua hiyo ya kuyaondoa mashitaka, kutokana na mamlaka aliyopewa kupitia Sheria ya Mwenendo wa Mashitaka ya Jinai nchini, Kifungu cha 91(1).

Hatua hiyo ilifuatiwa na maelezo ya Hakimu Luambano kwamba, kwa kuwa Mkurugenzi wa Mashitaka ameamua kuyaondoa mashitaka yote matano dhidi ya washitakiwa wote wanne, mahakama inaifuta rasmi kesi na kuwaachia huru washitakiwa.

“Mahakama hii inatamka kuwa washitakiwa mko huru kuanzia sasa,” alisema Hakimu Luambano, ambaye ameichukua kesi hiyo hivi karibuni baada ya kuwa ikisikilizwa mbele ya Hakimu Mkuu Mkazi, Thomas Simba.

Kwa mara ya kwanza kesi hiyo ilifikishwa mahakamani tarehe 14 Juni 2016.

Katika kesi hiyo, Lissu na wenzake walikuwa wanatuhumiwa kwa mashtaka matatu ya uchochezi, likiwemo la kutoa chapisho la uchochezi kwenye Gazeti la Mawio, toleo Na. 182 la tarehe 14 hadi 20 Januari 2016.

Shitaka jingine ni kupanga njama za kutoa chapisho la uchochezi, kosa walilodaiwa kutenda kati ya tarehe 12 na 14 Januari 2016, katika eneo lisilojulikana jijini Dar es Salaam, na Lissu na wahariri wa Mawio walidaiwa kupanga njama za kuchapisha taarifa za uchochezi.

Na shtaka la kuchochea hofu miongoni mwa wananchi kwa kuchapisha habari “Maafa yaja Zanzibar” na kwamba habari hiyo ilidaiwa ingeweza kuzua vita au umwagaji damu.

Uamuzi wa DPP kuondoa mashitaka ya uchochezi dhidi ya wahariri wa MAWIO, Mwanasheria Lissu na Mehboob wakati ikiwa imesita kuendelea na usikilizaji tangu pale Lissu aliposhambuliwa kwa risasi tarehe 7 Septemba 2017, akiwa kwenye shughuli za Bunge jijini Dodoma, na hivyo kuendelea kuwa nje ya nchi kwa ajili ya matibabu.

Mpaka Lissu alipopatwa na mkosi huo wa kushambuliwa kwa risasi kadhaa na hivyo kupata majeraha mazito yaliyomfikisha hadi Ubelgiji, upande wa mashitaka ulikuwa umewasilisha mashahidi wawili akiwemo Salum Hamduni, ambaye wakati huo alikuwa Mkuu wa Upelelezi wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Kipolisi wa Temeke, Dar es Salaam.

Hamduni sasa ni Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) nchini, uteuzi alioupata mwaka huu. Shahidi wa pili alikuwa John Hokororo aliyekuwa Msaidizi wa Mkurugenzi wa Idara ya Habari Tanzania (MAELEZO), akiwa ndiye Msajili wa Magazeti.

1 Comment

  • Yasikitisha mno kwawahusika watuhumiwa wa kesi kama hizi za uonevu kupita kiasi.

    Kiubinaadamu haijalishi ni upande gani wa siasa upo, lazima uone huruma kwa wahusika.

    Afrika demokrasia hatuiwezi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari Mchanganyiko

Mawakili waiburuza mahakamani TLS, EALS

Spread the love  WAKILI Hekima Mwasipu na wenzake wawili, wamefungua kesi katika...

Habari Mchanganyiko

Uvuvi bahari kuu wapaisha pato la Taifa

Spread the love  SERIKALI imesema uvuvi wa bahari kuu umeliingizia Taifa pato...

Habari Mchanganyiko

DPP aweka pingamizi kesi ya ‘watu wasiojulikana’

Spread the love  MKURUGENZI wa Mashtaka nchini (DPP), ameweka pingamizi dhidi ya...

Habari Mchanganyiko

Washindi saba safarini Dubai NMB MastaBata ‘Kote Kote’

Spread the loveKAMPENI ya kuhamasisha matumizi ya Mastercard na QR Code ‘Lipa...

error: Content is protected !!