October 5, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Dovutwa ang’ang’ana na uenyekiti wa UPDP 

Fahmi Nassoro Dovutwa, Mwenyekiti wa Chama cha United People's Democratic Party (UPDP)

Spread the love

FAHMI Nassoro Dovutwa, mwenyekiti wa taifa wa chama cha United People’s Democratic Party (UPDP), anayedaiwa kufukuzwa uongozi wa chama hicho, amegoma kuachia ngazi. Anaripoti Regina Mkonde…(endelea).

Anasema, “mimi bado ni mwenyekiti halali wa UPDP, niliyechaguliwa na mkutano mkuu wa taifa, miaka mitano iliyopita. Halmashauri kuu ya taifa, inayodaiwa imetumika kunifuta kazi, kwa mujibu wa katiba yetu, haina mamlaka hiyo.”

Anaongeza: “Hivyo basi, naomba kuwataarifu wanachama na viongozi wenzangu ndani ya chama chetu, kwamba taarifa zinazoenezwa na wakola, eti nimevuliwa uenyekiti, siyo za kweli.”

Anasema, “niwatoe wasiwasi wana UPDP wote nchini na waendelee na shughuli zao za ujenzi wa chama kwa kuwa chama chao, kiko kwenye mikono salama ya mwenyekiti Fahmi Nassoro Dovutwa.”

Kuibuka kwa mwanasiasa huyo, kukana madai kuwa amevuliwa uongozi wa chama hicho, kumekuja siku tatu, tokea makamu mwenyekiti wake upande wa Zanzibar, Abdalla Mohammed Khamis, kutangaza kuwa halmashauri kuu (NEC) ya UPDP, (NEC), iliyokutana mjini Unguja, imemvua uongozi Dovutwa.

 

Khamis alisema, Dovutwa amevuliwa wadhifa wake wa uenyekiti, kwa tuhuma za kukiondoa chama chake katika kinyang’anyiro cha uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji, bila ridhaa ya wanachama.

Akijibu madai hayo, Dovutwa anasema, “sisi ni chama huru. Ndani ya uongozi wangu, hatujawahi kushinikizwa kutamka wala kwa ishara, kususia uchaguzi.”

Alipoulizwa kama yeye hajashinikiza chama chake kususia uchaguzi, kwa nini sasa itangazwe kuwa amevuliwa uenyekiti; na kipi kimetokea mpaka yakaibuka madai hayo, Dovutwa anasema, “kwanza nikiri kuwapo kwa kikao cha NEC, lakini siyo kweli kwamba nimesimamishwa uongozi.”

Anasema, “…tarehe 1 Desemba 2019, tulikuwa na mkutano wa kawaida wa halmashauri kuu ya taifa. Ndipo katibu mkuu, Hamad Ibrahim, alibadili mwelekeo wa mkutano na kushawishi kupigwa kura kwa mwenyekiti kwa madai ya kuvunja katiba.

 

“Halmashauri kuu haina mamlaka ya kumchukulia hatua zozote mwenyekiti. Kazi ya halmashauri kuu, ni kumuondoa kiongozi aliyechaguliwa na chombo hicho. Mimi sijachaguliwa na halmashauri kuu. Nimechaguliwa na mkutano mkuu.”

Dovutwa anasema, “kwa mujibu wa katiba ya UPDP, Ibara ya 15, kifungu cha 5 (6), halmashauri kuu ya chama inaweza kumuondoa madarakani mtu waliyemchagua. Kazi ya halmashauri kuu, kama wana malalamiko juu yangu, ni kupelekea mapendekezo kwenye mkutano mkuu.”

 

Anasema, kutokana na matakwa hayo ya katiba, waliotangaza kumvua uenyekiti hawakuwa na mamlaka hayo na hivyo yeye bado anaendelea kutumikia nafasi yake.

Anasema, wote wanaompinga anawaomba wasubiri mkutano mkuu wa uchaguzi ili wajitokeze kugombea nafasi hiyo na wanachama ndio watakaoamua.

Wakati Dovutwa akiendelea kung’ang’aniza kuwa bado mwenyekiti wa chama hicho, katibu mkuu wake huyo – Hamad Ibrahim – anasema, “Dovutwa ameandikiwa barua ya kuvuliwa uenyekiti na kufukuzwa uanachama, tokea jana tarehe 4 Desemba 2019.”

Katika barua hiyo iliyotumwa kwa Dovutwa, Hamad anasema, Dovutwa amejulishwa kuvuliwa uenyekiti na kufukuzwa uanachama wa UPDP, kupitia kikao cha halmashauri kuu kilichofanyika, tarehe 1 Desemba 2019, Visiwani Zanzibar.

Tuhuma za Dovutwa zilizoandikwa kwenye barua hiyo, ni pamoja na kushindwa kujaza nafasi ya Naibu Katibu Mkuu kwa zaidi ya mwaka mmoja, na kujitoa kushiriki uchaguzi wa Serikali za Mitaa bila idhini ya Kamati Kuu ya chama chake.

error: Content is protected !!