August 16, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Dovutwa aivaa Ukawa

Spread the love

FAHMI Dovutwa, Mwenyekiti wa Chama cha United Peoples Democratic Party (UPDP) amekosoa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kwa madai, mfumo wake hautoi nafasi kwa watu wengi kufanya uamuzi, anaandika Happiness Lidwino.

Akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam jana Dovutwa amedai, hoja za Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chadema pia Mweneyekiti Mwenza wa Ukawa za kususia hotuba ya bajeti ya Waziri Mkuu ni za msingi na zimeiva vya kutosha.

Na kwamba, kitendo cha kuondoka na hoja zake nje amedai kinaonesha mfumo wa uongozi wa Ukawa ni wa mtu mmoja.

Jumamosi wiki iliyopita, Freeman Mbowe baada ya kusoma hotuba kuhusu makadirio ya mapato na matumizi ya fedha katika Ofisi Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2016/17 alitoka nje na kuzungumza na waandishi wa habaru kuwa, kasoro zilizofanya wachukue uamuzi huo ni kukiuka masuala ya kisheria katika utekelezaji wa bajeti, kutotangaza kwenye Gazeti la Serikali mabadiliko ya wizara na kutorushwa kwa vipindi vya Bunge kwenye televisheni.

Alitaja hoja nyingine kuwa ni uvunjwaji wa Katiba na sheria za nchi kuhusiana na bajeti unaofanywa na serikali pamoja na kuminya uhuru na madaraka ya mhimili wa Bunge kwa kuzuia matangazo ya wasusia Bunge kurushwa moja kwa moja na vituo vya televisheni.

“Hatutashiriki mjadala tunaendelea kutafakari hatua nyingine za kuchukua kama Serikali na Bunge hawatatafuta ufumbuzi wa masuala hayo matatu,” alinukuliwa Mbowe.

Kwenye mkutano wake Dovutwa amedai, Ukawa una udhaifu mkubwa wa kujenga hoja kwa kutegemea mazingira na wakati, na kwamba kitendo chao cha kutoka ndani ya Bunge kwa msimamo wa kugomea hotuba ya bajeti ya Waziri Mkuu, “inaonesha wazi ni namna gani serikali ilikuwa sahihi kusitisha matangazo ya Bunge ya moja kwa moja.”

“Kwa sababu kodi za Watanzania haziwezi kuwa zinatumika kwa kufanya vibweka bungeni, Watanzania wanatarajia wabunge waliowachagua watakuwa ni sauti ya kuwapigania mipango yao ndani ya bunge sambamba na kuwatetea pale itakapobidi,” amesema.

Amesema, endapo uwepo wa Ukawa bungeni ungekuwa unazingatia kinachozungumzwa ndani ya Bunge, wasingeshangazwa kusitishwa kwa matangazo ya moja kwa moja.

“Mjadala wa kusitisha matangazo ya moja kwa moja ya bunge na uanzishwaji wa studio ya kurekodi na kurusha matangazo ya bunge ulijadiliwa katika bajeti ya mwaka 2015/16 na fedha zimetengwa kwa ajili hiyo. Hivyo kususa kwao kunaonesha jinsi gani Ukawa huwa makini na mambo wanayoyataka tu,” amesema.

Pia amewataka Ukawa kubadilika kwa kuanza kutafakari zaidi badala ya kufanya siasa kwa historia.

“Kitendo chao cha kuondoka bungeni si cha kiungwana kwani kinawanyima nafasi wapiga kura wao kuwa na wasemaji,” amesema.

Hata hivyo Dovutwa amemtaka Job Ndugai, Spika wa Bunge kuwaeleza Watanzania vigezo vinavyowezesha wabunge wasiofanya kazi wasilipwe posho.

error: Content is protected !!