KAMAMU Mwenyekiti wa Chama cha ACT-Wazalendo Bara, Dorothy Semu amekaimu rasmi kiti cha uenyekiti wa chama hicho, kilichokuwa kikishikiliwa na Hayati Maalim Seif Sharif Hamad, aliyefariki dunia hivi karibuni. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).
Maalim Seif, aliyekuwa mwenyekiti wa chama hicho Taifa, alifariki dunia tarehe 17 Februari 2021 katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), jijini Dar es Salaam ambapo mwili wake ulizikwa tarehe 18 Februari 2021 kijijini kwao Nyali-Mtambwe, Kisiwani Pemba.
Taarifa ya Semu kukaimu nafasi ya Hayati Maalim Seif, imetolewa Jumatatu tarehe 22 Februari 2021 na Katibu wa Habari, Uenezi na Mahusiano na Umma ACT-Wazalendo, Salim Bimani.
Taarifa ya Bimani imesema, hatua hiyo ni matakwa ya Ibara ya 84 (3) na (4) ya Katiba ya ACT-Wazalendo ya 2015, Toleo la 2020.

“Ibara hiyo inasomeka kama ifuatavyo, 84 (3); iwapo mwenyekiti wa chama hayupo kwa sababu yoyote ile basi makamu mwenyekiti ambaye anatoka upande mwingine wa muungano tofauti ns anaotoka mwenyekiti, na kama makamu mwenyekiti aliyetajwa kwanza naye hayupo, basi makamu mwenyekiti aliyebakia atakaimu nafasi ya uenyekiti,” imesema taarifa ya Bimani.
Kwa mujibu wa taarifa ya Bimani, Semu atakaimu nafasi hiyo katika kipindi kisichozidi miezi 12, hadi pale Mwenyekiti mpya atakapochaguliwa na Mkutano Mkuu Maalumu wa Taifa.
“Kwa kuzingatia Ibara ya 84 (4) ya Katiba ya ACT-Wazalendo, Dorothy Semu ataendelea kukaimu nafasi hiyo kwa kipindi kisichozidi miezi 12 hadi pale mwenyekiti moya atakapochaguliwa na Mkutano Maalumu wa Taifa,” imesema taarifa ya Bimani.
Hayati Maalim Seif alichaguliwa na ACT-Wazalendo kuwa mwenyekiti wa chama hicho tarehe 14 Machi 2020, nafasi aliyoitumika hadi umauti ulipomkuta.
Leave a comment