January 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Don Bosco yaandaa kampeni maalum

Spread the love

TAASISI ya Don Bosco Net imeandaa kampeni maalum ya kuhamasisha wasichana kushiriki na kupenda mafunzo ya ufundistadi yenye lengo la kutatua changamoto na kutumia fursa za kujiendeleza. Anaandika Hamisi Mguta … (endelea).

Hayo yamesemwa leo Jijini Dar es Salaam na viongozi wa tasisi ya Don Bosco Net wakati wakitoa taarifa ya uzinduzi wa kampeni hiyo iliyopewa jina la ‘Binti thamani kampeni’.

Mratibu wa kampeni hiyo, Agnes Mgongo amesema kwa upande wa Dar es Salaam kampeni zitahitimishwa Novemba 17 mwaka huu katika ukumbi wa King Solomon na kwa upande wa Dodoma zitahitimishwa Novemba 28, katika ukumbi wa Don Bosco Technical School.

Mgongo ambaye pia ni Mkurugenzi wa Trumark ambao ndio waratibu wa kampeni hiyo amesema, kampeni hiyo itawasaidia wasichana kutambua kuwa wao ni taifa kubwa na wanategemewa kwani kesho yao inajengwa na leo yao.

Mkurugenzi wa vijana wa tasisi ya Don Bosco Net, Dunstan Haule amesema taasisi hiyo inahimiza jamii kutambua kuwa wasichana wana fursa za kujiunga na masomo ya ujasiriamali katika vituo vyote vilivyopo Tanzania vya Don Bosco kwa gharama nafuu.

Haule amesema sanjari na hayo Don Bosco Net kupitia vyuo vyao vya ufundi imekuwa ikitoa kozi mbalimbali ambazo ni ushonaji, umeme, mafunzo ya kompyuta, uchomeleaji, kuranda pamoja na ujenzi.

“Kampeni hii itawakinga wasichana wapatao 2,000 pamoja na wadau mbalimbali wakiwemo wazazi, walimu na marafiki wa Don Bosco kuhakikisha uhamasishaji unafanikiwa,” amesema Haule.

Kampeni hiyo iliyo chini ya udhamini wa DBNETT, Serikali ya Ubeligiji kupitia taasisi yao ya VIA Don Bosco, Hugo Domingos na King Solomon Hall itasindikizwa na burudani kutoka kwa msanii Barnaba pamoja na Mshereheshaji na mchekeshaji MC Pilipili.

Wengine wanaotarajiwa kuwepo ni pamoja na wale waliofanikiwa kupitia ufundi stadi, pia chakula na vinywaji kwa wanafunzi, wazazi na walimu vitatolewa.

error: Content is protected !!