August 15, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Dodoma yazingirwa, Bavicha wawindwa

Spread the love

MJI wa Dodoma umezingirwa na Jeshi la Polisi. Gari la maji ya kuwasha na yaliyobeba polisi muda huu ndiyo yanayoonekana kwa wingi kwenye maeneo mbalimbali tofauti na ilivyo kawaida, anaandika Dany Tibason.

Polisi wanaonekana kuwa tayari kwa lolote, wamejaa kwenye magari yao huku wakizunguka maeneo mbalimbali ya Mji wa Dodoma sambamba na gari la maji ya kuwasha ili kukabiliana na kile kinachojulikana kuwa ni vijana wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo Chadema (Bavicha).

Kwa wiki mbili sasa kuna kutupiana maneno kati ya Jeshi la Polisi, Bavicha na Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) kuhusu kufanyika kwa Mkutano Mkuu wa CCM mjini Dodoma wiki mbili zijazo.

Bavicha wamedhamiria kuzuia mkutano huo uliolenga kukabidhiwa uenyekiti wa CCM kwa Dk. John Magufuli kutoka kwa mwenyekiti wa sasa, Dk. Jakaya Kikwete.

Awali, Jeshi la Polisi lilipiga marufuku mikutano yote ya hadhara na ya ndani ya vyama vya siasa, hali ambayo imeathiri mikutano ya Chadema hivyo Bavicha kudhamiria mkutano wa CCM kutofanyika. Marufuku ya mikutano ya kisiasa ilianza kutolewa na Rais Magufuli.

Kutokana na dhamira hiyo, UVCCM walionya mkutano wao kutoingiliwa na yoyote, hata hivyo Jeshi la Polisi limeshindwa kuzuia mkutano huo huku wakibadili kauli kwamba, mikutano ya ndani haikuzuiliwa.

Bavicha wamedhamiria kukutana Dodoma ‘kuisaidia’ polisi kuvuruga mkutano huo, hata hivyo polisi inatetea mkutano huo.

Mjini Dodoma leo, wananchi wamelazimika kusimamisha shughuli zao na kushangaa magari zaidi ya 20 yakiwemo ya kuwasha, magari ya askari wa mbwa na askari wengi wakiwa na sare zao, silaha za moto pamoja na mabomu ya machozi.

Kwa mujibu wa Lazaro Mambosasa, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma amedai, ni mazoezi ya kawaida ambayo wameamua kuyafanya muda wa mchana badala usiku kama walivyozoea.

Mambosasa amesema, wamelazimika kufanya mazoezi kwa kutumia vifaa vya kipolisi ili wananchi waweze kutambua kuwa, Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma lipo imara zaidi.

Amesema, mazoezi hayo ni sehemu tu ya mazoezi huku akitamba kuwa, Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma lipo imara “na asiwepo mtu yoyote ambaye atajaribu kuingilia kazi za polisi.”

“Wale wote ambao watajipendekeza kwa madai ya kutaka kulisaidia Jeshi la Polisi, watakipata cha mtema kuni,” amesema na kuongeza;

“Hakika nataka kuwaeleza wananchi, asiwepo mtu wa kujaribu kwani tutawakamata na ijulikane wazi kuwa, kuingia rumande ni rahisi lakini kutoka itakuwa ngumu.”

Patrick Ole Sosopi, Makamu Mwenyekiti wa Bavicha Taifa amesema, kitendo cha Jeshi la Polisi kuzunguka mji mzima kwa kuonesha vifaa vyao vya kivita ni dalili za uoga.

“Kitika kitendo ambacho kimefanya na Jeshi la Polisi ni dalili uoga na inaonesha ni jinsi gani Bavicha walivyo na nguvu kiasi cha kulitikisa jeshi hadi kufikia hatua ya kufanya vitisho,” amesema Sosopi.

error: Content is protected !!