July 6, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Dodoma washauriwa kuachana na mahindi

Spread the love

WAKULIMA wa mkoani Dodoma wameshauriwa kuacha kulima zao la mahindi na badala yake walime mazao mengine yanayoendana na hali ya hewa ya kanda ya kati. Anaandika Dany Tibason, Dodoma … (endelea).

Aidha, imeelezwa kwamba mkoa wa Dodoma umekuwa ukikumbwa na baa la upungufu wa chakula kila mwaka kutokana na wakulima kushindwa kulima mazao ambayo yanastawi katika kanda yao.

Akiongea na MwanaHALISI Online, Afisa Kilimo ya mkoa, Abramu Isack amesema hali ya hewa iliyopo mkoani hapa siyo rafiki kwa kilimo cha mahindi.

“Kwa muda mrefu wakulima mkoani Dodoma wamekuwa wakiwekeza nguvu kubwa na fedha nyingi katika kilimo cha mahindi bila mafanikio kwa sababu ya kushindwa kupata taarifa za kitaalamu. Mkoa wa Dodoma hauna mvua wala hali ya hewa inayoweza kustawisha zao la mahindi,” amesema.

Akieleza kitaalamu zaidi, Abramu amesema, ili zao la mahindi listawi linahitaji kiwango cha mvua cha kati ya milimita 1,800 hadi 2,200 kwa mwaka wakati mkoa wa Dodoma unatabia ya mvua ya kati ya milimita 400 hadi 800 kwa mwaka.

“Kwa hali hii ni wazi kabisa kwamba kanda ya kati siyo kanda inayostawisha mahindi hivyo ni vyema wakulima sasa wakaanza kulima mazao yanayosistawi hapa badala ya kupotezamuda na fedha zao,” alieleza.

Alitaja baadhi ya mazao ya biashara yanayostawi vizuri mkoani Dodoma kama mtama, uwele, zabibu, ufuta na karanga. “Wakulima wengi wanan’gan’gania kulima mahindi kwa kuogopa njaa, lakini kumbe wanaweza kulima mazao haya ya biashara na baadaye kuyauzana hatimaye wakanunua mahindi kwa ajili ya chakula,” aliongeza.

Hata hivyo, amezitaka baadhi ya taasisi zisizo za kiserikali kuacha tabia mbaya ya kuwahamasisha wakulima wa Dodoma kulima zao la mahindi pasipo kuwa na takwimu za kitaalamu juu ya ustawi wa zao hilo mkoani hapa.

Dodoma ni miongoni mwa mikoa ambayo imekuwa ikikumbwa na baa la upungufu wa chakula kila mwaka kutokana na mavuno kidogo yanayopatikana miongoni mwa wakulima.

error: Content is protected !!