MASHINDANO ya Ngoma za Jadi ‘Tulia Traditional Dances Festival’ yanayohusisha tamaduni kutoka mikoa mbalimbali yataanza Alhamisi hii tarehe 23 hadi 25 Septemba 2021 jijini Mbeya nchini Tanzania. Anaripoti Patricia Kighono, TUDARCo … (endelea).
Mwandaaji wa mashindano hayo ni Mbunge wa Mbeya Mjini (CCM) ambaye pia ni Naibu Spika wa Bunge la Tanzania, Dk. Tulia Ackson ambaye amewaeleza waandishi wa habari leo Jumanne, tarehe 21 Septemba 2021 waandamizi kuwa yamekamilika.
Dk. Tulia amesema, mashindano hayo ni tukio kubwa la kihistoria ambalo kwa miaka minne mfululizo limekuwa likifanyikia katika Wilaya ya Rungwe na mwaka huu “tumeamua kulileta ndani ya Jiji la Mbeya nalo si lingine bali ni Tulia Traditional Dances Festival.”
Amesema mashindano hayo yanakutanisha tamaduni kutoka mikoa yote nchini ambapo washiriki wanashindanishwa uwezo wao na washindi wanapewa zawadi mbalimbali huku lengo kuu likiwa ni kuuenzi utamaduni wetu.

Mashindano hayo pia yana lengo la kutengeneza fursa za kiuchumi kwa wananchi ambao kupitia mashindano hayo watawezankufanya biashara zao
Aidha, msanii maarufu nchini humo, Raymond Mwakyusa maarufu Rayvanny atakuwa miongoni mwa washiriki kutumbuiza siku ya ufunguzi na kuzungumza na baadhi ya wasanii ili kuwapa mwanga wa kufikia mafanikio.
“Mtoto wetu Rayvanny naye atakuwepo siku ya ufunguzi kwa ajili ya kutumbuiza na hata kuzungumza na baadhi ya wasanii wetu wa hapa Mbeya kwa lengo la kuwaonesha njia nzuri ya kuyafikia mafanikio,” amesema Dk. Tulia
Amesema, mashindano hayo yanakusudia kuleta fursa nyingi ikiwemo za utalii katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini hivyo wanatarajia uwepo wa baadhi ya viongozi wa Serikali wakiwemo Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Damas Ndumbaro pamoja na Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Innocent Bashungwa.
Amewaomba wananchi kujitokeza kwa wingi katika shindano hilo
Leave a comment