May 27, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Dk. Tulia kumrithi Ndugai, CCM yafyeka 69

Dk. Tulia Ackson, Spika wa Bunge la Tanzania

Spread the love

 

KAMATI Kuu ya chama tawala nchini Tanzania – Chama Cha Mapinduzi (CCM), imempitisha Dk. Tulia Ackson kuwa mgombea wa kiti cha Spika wa bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma  … (endelea).

Hatua hiyo imekuja baada ya Kamati hiyo kuchukua jukumu zito la kuchekecha 70 waliojitosa kumrithi Job Ndugai aliyejiuzulu nafasi hiyo tarehe 6 Januari Mwaka huu.

Akizungumza na waandishi wa habari Katibu wa NEC – Itikadi na Uenezi- CCM, Shaka Hamdu Shaka amesema Dk. Tulia ambaye pia ni Naibu Spika wa Bunge hilo, amepitishwa kwa kura za kutosha kuwania nafasi hiyo. 

Kamati hiyo iliyokuwa chini ya Mwenyekiti wake, Rais Samia Suluhu Hassan, ilikutana jana kufanya mchujo huo ambao mwisho wake wagombea 69 wamepigwa chini.

Wagombea wote hao, walijitokeza kuwania kuvaa joho la uspika wa Bunge la Tanzania, baada ya Job Ndugai ambaye alijiuzulu nafasi hiyo tarehe 6 Januari 2022.

Alichukua uamuzi huo, baada ya kauli yake aliyoitoa kuhusu serikali kuendelea kukopa fedha nje kuibua mjadala mkali ndani ya chama chake na kushinikizwa kujiuzulu.

Kamati hiyo, imekutana ikiwa ni siku mbili zimepita tangu sekretarieti ya chama hiyo, chini ya uenyekiti wa Katibu Mkuu wa CCM, Daniel Chongolo kujadili wagombea na kuishauri kamati kuu hiyo.

HAKUNA WAGOMBEA WATATU

Ratiba iliyotolewa na CCM ya mchakato mzima, mara baada ya kamati kuu kukamilisha kazi yake, ilitakiwa kuteua wagombea watatu ambao hao wangekwenda kupigiwa kura na kamati ya wabunge wote wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Hata hivyo, utaratibu huo umeonekana kuwekwa kando na sasa amepitishwa Dk. Tulia moja kwa moja.

  1. TULIA NI NANI

Tulia Ackson ambaye amezaliwa tarehe 23 Novemba 1976), ni mwanasheria na mwanasiasa Mtanzania na mwanachama wa ChamaCha Mapinduzi (CCM).

Aliteuliwa na Rais John Magufuli kuwa mbunge kwa miaka 2015 – 2020 kisha akachaguliwa pia kuwa naibu spika.

Ackson alizaliwa kwenye kata ya Bulyaga, Tukuyu kwenye wilaya ya Rungwe. Alisoma shule huko Tukuyu na Mbeya.

Dk. Tulia Ackson

Miaka 1998-2003 alisoma sheria kwenye chuo kikuu cha Dar es Salaam akaendelea kusoma kwa shahada ya uzamivu huko Cape Town, Afrika Kusini miaka 2005-2007.

Alirudi Dar es Salaam alipofundisha sheria kwenye Chuo kikuu  cha Dar es salaam hadi mwaka 2014 alipoteuliwa na rais Jakaya Kikwete kuwa mjumbe wa Bunge Maalum la Katiba. Mwaka 2015 alikuwa kati ya wabunge 10 walioteuliwa na rais kuingia bungeni.

WALIOKATWA KUWANIA UNAIBU?

Hata hivyo, baada ya Dk. Tulia kupitishwa kuwania nafasi ya Spika, ni dhahiri kwamba atatakiwa kujiuzulu nafasi ya Unaibu Spika.

Hivyo, nafasi hiyo itakuwa wazi na mchakato wake utaanza mapema ili Bunge hilo  lianze shughuli zake Februari mwaka huu.

WALIOKATWA HAWA HAPA

Aidha, vigogo wa Bunge, mawaziri wastaafu, wanasheria, wasomi na wanachama wa kawaida walijitosa kwenye mbio hizo ambazo wote 70 wamepitishwa katika chujio la kumpata Dk. Tulia atakayekwenda kushindanishwa na wa vyama vingine.

Kati ya waliokuwa wamejitosa kwenye mbio hizo, mbali na Naibu Spika, Dk. Tulia Ackson, wengine walikuwa Mwenyekiti wa Bunge, Mussa Zungu na waliowahi kuongoza Bunge kwa maana ya mwenyekiti, Andrew Chenge ambaye amewahi kuwa mwanasheria mkuu wa serikali.

Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashililah naye ni miongoni mwa waliokuwa wamechukua fomu akitaka kurejea kwenye uongozi wa muhimi huo pamoja na Asia Abdallah, Angelina John na waziri wa zamani katika serikali ya awamu ya nne aliyehudumu pia nafasi ya mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa chama hicho Taifa (UWT), Sophia Simba. 

    Andrew Chenge

Aidha, walikuwemo wabunge, Joseph Msukuma wa Geita Vijijini, Godwin Kunambi wa Mulimba mkoani Morogoro, Luhaga Mpina wa Kiseka mkoani mwanza pamoja na Emmanuel Mwakasaka waTabora Mjini ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge.

Kuna mawaziri wa zamani wa mifugo na uvuvi, Dk. Titus Kamani ambaye mwaka 2015 alikuwa kati ya wanachama 38 wa CCM waliochukua na kurejesha fomu ya kuwania urais ndani ya chama hicho lakini hakufanikiwa.

Aliyewahi kuwa naibu waziri wa nishati na madini wakati wa utawala wa awamu ya nne wa Jakaya Kikwete akiwakilisha wananchi wa Shinyanga Mjini, Stephen Masele naye alichukua fomu. 

Stephen Masele, Makamu Rais wa Bunge la Afrika Mashariki (PAP)

Masele amewahi kuwa Makamu wa Kwanza waRais wa Bunge la Afrika (PAP). 

Katika hao 69, kuna msomi mwenye shahada mbalimbali tisa kutoka vyuo vya ndani na nje ya Tanzania, Profesa Handley Mafwenga. 

Wengine kwenye waliokuwa kwenye kinyang’anyiro hicho ni, Dk. Saimon Ngatunga, Tumsifu Mwansamale, Merkion Ndofu, Ambwene Kajula, Patrick Nkandi, Hamidu Chamani na Goodluck Ole-Madeve. 

Pia, walikuwemo Juma Chum, Baraka Byabato, Dk Musa Ngonyani, Faraji Rushagama, Hamisi Rajabu, Festo Kipate, George Nangale, Barua Mwakilanga, Zahoro Hanuna  na Thomas Kirumbuyo na Mhandisi AbdulAziz Jaad Hussein.

Mbio hizo zimewashuhudia wengine waliokuwa wamejitosa kama Hatibu Mgeja, Dk. Linda Ole Saitabau na Mbunge wa zamani wa Makete, Profesa Norman Sigalla King, Emmanuel Sendama, Bibie Mssumi, Hilal Seif, Athumani Mfitakamba, Mwenda Mwenda na Mbunge wa zamani wa Ulanga, Goodluck Mlinga. 

Wengine walikuwa, Herry Kessy, Josephat Malima, Adam Mnyavanu, Andrew Kevela na Mbunge wa Nyasa, Stella Manyanya.

error: Content is protected !!