August 15, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Dk. Tulia asota Dodoma

Spread the love

Dk. Tulia Ackson, Naibu Spika wa Bunge anaonja maumivu kutoka kwa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), anaandika Dany Tibason.

Kila anapokuwepo Dk. Tulia, Ukawa wanaondo na hata kusababisha protokali kuvurugika. Ni kwa kuwa, Ukawa wameweka msimamo wa kutoshirikiana ama kutoshiriki shughuli ambayo yeye (Dk. Tulia) anashiriki.

Hivi ndivyo ilivyotokea leo katika ukumbi wa Chuo cha Mipango mjini Dodoma muda mfupi baada ya Kasimu Majaliwa, Waziri Mkuu kumaliza kuzindua Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano.

Baada ya Waziri Mkuu kumaliza hotuba yake na kufuatia zoezi la ugawaji vitabu vinavyoelezea mpango huo kwa ajili ya kujisomea katika taasisi na baadhi ya viongozi mbalimbali.

Katika uzinduzi huo mshehereshaji aliyefahamika kwa jina moja la Mzee Mavunde, alianza kuita viongozi mbalimbali ili kuchukua vitabu kwa ajili ya taasisi ama makundi yao.

Ulipofika wakati wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kwenda kuchukua kitabu kuwakilisha kambi hiyo, mshereheshaji alimwita mnadhimu mkuu wa kambi hiyo ambapo hakutokea.

Baada ya kuonekana kwamba, hakuna anayejitokeza kupokea kitabu hicho, haraka haraka Steven Hillary Ngonyani,Mbunge wa Korogwe Vijijini maarufu kwa jina la Prof. Maji Marefu alichomoka moja kwa moja na kwenda kupokea kitabu cha mpango huo wa miaka 5 kwa niaba ya kambi ya upinzani bungeni.

Kitendo hicho kiliwafanya wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambao walikuwa ukumbini hapo pamoja na wageni wengine kuangua kicheko.

Ukawa wamekuwa wakitoka bungeni pale Dk. Tulia anapoongoza bunge hilo. Hatua hiyo inatokana na malalamiko yao kwamba, kiongozi huyo wa Bunge anaendesha taasisi hiyo kwa kupendelea CCM.

 

error: Content is protected !!