August 17, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Dk. Tulia apigania wanawake, watoto

Spread the love

 

WABUNGE wa Jumuiaya ya Ustawi wa Maendeleo ya nchi zilizopo Kusini mwa Afrika (SADC) wamekutana mjini Dodoma kujenga uhusiano wa karibu ikiwa ni pamoja na kujadili kuhusu maradhi ya UKIMWI, anaandika Dany Tibason.

Hatua hii imekuja wakati wadau mbalimbali wa masuala ya afya wakipigania kuhakikisha ugonjwa huu unapungua au kutoweka kabisa kwa manufaa ya ustawi wa jamii.

Dk. Tulia Ackson ambaye alikuwa mgeni rasmi akimwakilisha Joab Ndugai, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amewahimiza wajumbe hao kushirikiana kwa pamoja kujadili jinsi watakavyozishauri serikali zao kuondoa maambukizi mapya.

Amesema kuwa, mbali na kwamba kuna maambukizi mapya, dunia inapaswa kujua kuwa wanaoathirika zaidi ni wanawake na watoto.

“Dunia inapaswa kuwajali zaidi wanawake na watoto kwa kuwa, ndio wanaoathirika zaidi na maambukizi ya Ukimwi.

“Kila mmoja kwa wakati wake tunalazimika kuukemea unyanyapaa unaoathiri kundi hili na kusababisha kukata tamaa,”amesema.

Hata hivyo, Dk. Tulia amesema unyanyapaa uliopo sehemu za kazi unapunguza malengo ya maendeleo ya kila nchi na hivyo ni wajibu wa kila mfanyakazi kwa nafasi yake kuonesha kujali hisia za wengine.

Wakati huo huo Dk Hamis Kigwangala, Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii amebainisha kuwa, kila mtu ana haki ya kupata huduma bora ya afya na kuwataka wajumbe wa SADC kupeleka ujumbe kwenye nchi zao juu ya uhuru  wa huduma bora bila kubaguliwa.

Aidha, ametaja huduma ya uzazi salama na usawa katika jamii kuwa ni moja ya malengo yatakayoweza kuleta maendeleo  ya huduma ya afya ya uzazi na kwamba kufikia mwaka 2030 nchi ya Tanzania itahakikisha imetimiza malengo hayo.

“Huduma ya uzazi salama inahitajika kuwalinda wanawake dhidi ya maambukizi mapya na hivyo malengo ya mwaka 2030 nchini Tanzania itahakikisha inatimiza ili kuleta usawa wa huduma katika jamii,”amesema.

 

error: Content is protected !!