July 6, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Dk. Slaa “avamiwa”

Dk. Willibrod Slaa
Spread the love

WATU ambao hadi sasa hawajafahamika wameingilia mawasiliano ya Dk. Willibrod Slaa kwenye mtandao wa intaneti na kuchukua nyaraka mbalimbali, imefahamika.

Vyanzo vya taarifa vinasema, mawasiliano ya Dk. Slaa yaliingiliwa kati ya 17 na 25 Septemba 2013, wakati akijiandaa kwenda nchini Marekani.

Dk. Slaa amethibitishia gazeti hili kuingiliwa mawasiliano yake na kusema, aligundua kuingiliwa huko kwenye mtandao wake, tarehe 22 Septemba 2013.

“Niliambiwa kuwa walioniingilia walikuwa Baltimore, Marekani. Wakati napokea ujumbe kunifahamisha mawasiliano yangu kuingiliwa, tayari mimi nilikuwa nimefika Marekani,” ameeleza.

Dk. Slaa alikuwa Marekani kwa wiki tatu ambako, pamoja na mengine, alikutana na viongozi mbalimbali wakiwamo wabunge na maseneta.

Anasema kwa mujibu wa ujumbe aliopokea kutoka kwenye imeili yake, wadokozi hao wa mawasiliano yake walishindwa kuambulia chochote cha maana kutoka kwake.

Hii si mara ya kwanza mawasiliano ya Dk. Slaa kuingiliwa. Mwaka 2009, watu wanaodhaniwa kuwa maofisa usalama wa taifa (TISS), waliingilia mawasiliano ya kiongozi huyo mkuu wa upinzani nchini na kufanikiwa kuchukua nyaraka mbalimbali za chama chake.

Miongoni mwa nyaraka ambazo zilichukuliwa kwenye imeili ya Dk. Slaa miaka mitatu iliyopita, ni pamoja na taarifa za akaunti ya benki zinazomuhusu kigogo mmoja mwandamizi serikalini anayetuhumiwa kwa ufisadi.

Haikuweza kufahamika mara moja, akaunti hiyo ya kigogo wa serikali ilikuwa ni kutoka benki gani na kiasi gani cha fedha kilikuwa kwenye akaunti hiyo.

Uchunguzi wa jarida hili umegundua walioingilia mawasiliano ya Dk. Slaa, walifanya hivyo kwa msaada wa mtalaamu wa kompyuta (IT) aliyeko nchini China. Haikuweza kufahamika mara moja uraia wa mtu huyo wala jina lake.

Kwa mujibu wa vyanzo vya taarifa, kudokolewa kwa mawasiliano haya ya majuzi ya Dk. Slaa, kuligunduliwa kwa mara ya kwanza na ofisa mmoja wa serikali ambaye ni swahiba wa kiongozi huyo.

Mfanyakazi huyo wa ngazi ya juu serikalini ndiye aliyemjulisha Dk. Slaa kuingiliwa kwa mawasiliano yake na kumueleza wadokozi wa mawasiliano walikuwa wanatafuta taarifa juu ya ziara yake nchini Marekani.

“Salaam, nimemjulisha Dk. Slaa kuhusu kuingiliwa kwa mtandao wake. Nasikitika mpaka sasa hajanijibu. Tafadhali naomba umjulishe juu ya jambo hili na kumuomba aondoe nyaraka zote nyeti kwenye imeili yake kama bado zipo,” ameeleza msiri huyo wa Dk. Slaa kwenye ujumbe uliopitia kwa mtu mwingine.

Vyanzo vya taarifa kutoka watu waliokaribu na kiongozi huyo vinasema, miongoni mwa vitu vilivyokuwa vimehifadhiwa kwenye imeili ya Dk. Slaa, ni pamoja na nyaraka nyeti zinazohusu ununuzi wa samani za ofisi moja nyeti ya serikalini jijini Dar es Salaam.

Samani hizo zenye kugharimu mamilioni ya shilingi, zinaelezwa kuwa zimepangwa kununuliwa nchini Afrika Kusini.

Nyaraka nyingine ni kuhusu mkataba wa ujenzi wa kituo cha kuzalisha umeme cha Kinyerezi, jijini Dar es Salaam, ambacho kinatajwa kuwa na uwezo wa kuzalisha megawati 240.

Nyaraka zilizokutwa kwenye imeili ya Dk. Slaa, uchunguzi wa MwanaHALISI Online unaonyesha, zinahusu pia mkataba wa Kinyerezi uliopewa kichwa cha maneno, “Memorandum for Kinyerezi 240MW Combined Cycle Power Plant Project.”

Mkataba wa Kinyerezi, nyaraka zinaonyesha, ulifungwa Mei 2013 kati ya Wizara ya Fedha na Uchumi, Shirika la Umeme la Taifa (TANESCO) kwa upande mmoja na Japan Bank for International Cooperation (JBIC), Nippon Export and Investment Insurance (NEXI) na Sumitomo Mitsui Banking Corporation.

Kingine ambacho kilihifadhiwa kwenye imeili hiyo, ni taarifa ya uchunguzi wa nyara za serikali uliofanywa na kinachoitwa, “Kitengo cha Intelejensia” kutoka hifadhi za taifa za Tanapa.

Nyaraka nyingine, ni kuhusu ujangili kwenye hifadhi za Mikumi mkoani Morogoro, Ruaha pamoja na mawasiliano kati yake na viongozi wenzake kwenye chama na wabunge.

Dk. Slaa ndiye anatajwa kuwa mwanasiasa shupavu anayekinyima usingizi Chama Cha Mapinduzi (CCM), kwenye kinyang’anyiro cha urais mwaka 2015.

Dk. Slaa aligombea urais kwa mara ya kwanza katika uchaguzi mkuu uliopita ambapo alikuwa wa pili baada ya Rais Jakaya Kikwete aliyetangazwa mshindi.

Kana kwamba Freeman Mbowe alikuwa anapima upepo, mapema mwaka huu, alimtangaza Dk. Slaa kuwa mgombea wa chama hicho kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.

“Hatutafuti mgombea. Sisi tayari tunaye mgombea wetu. Ni Dk. Willibrod Peter Slaa. Muda ukifika tutafanya taratibu za kumpitisha,” alisema Mbowe kwenye mkutano mkubwa wa hadhara mjini Karatu.

Jarida hili lilipomuuliza katibu mkuu huyo wa CHADEMA, ni nyaraka zipi zilikuwapo kwenye imeili yake, haraka alisema, “Kulikuwa na vitu vya kawaida tu.”

Alipoelezwa kama kulikuwa na vitu vya kawaida kwa nini anadhani wamempekua, yeye alisema, “Yawezekana walikuwa wako kazini.”

Alipoulizwa kwamba haogopi kwa kuwa sasa mawasiliano yake yote yatakuwa yamevuja, Dk. Slaa alijibu, “Siogopi. Sina cha kuficha.”

error: Content is protected !!