January 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Dk. Slaa abwaga manyanga CHADEMA

Spread the love

ALIYEKUWA Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk Willibrod Slaa ametangaza rasmi kuachana na siasa. Anaandika Pendo Omary … (endelea).

Amesema hatua hiyo inatokana na hatua ya CHADEMA kumkaribisha Edward Lowassa bila masharti na baadaye kumteua kuwa mgombea urais wa chama hicho.

Lowassa ambaye ni mgombea urais wa CHADEMA, anaungwa mkono na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) ambavyo ni CHADEMA yenyewe, CUF, NCCR-Mageuzi pamoja na NLD.

Katika mkutano wake na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Dk. Slaa amesema hatojiunga na chama chochote cha siasa na badala yake ataendelea kuwatumikia wananchi nje ya siasa.

Hata hivyo amesema uamuzi huo unatokana na kutoridhishwa na hatua zilizochukuliwa na viongozi wakuu wa CHADEMA akiwemo mwenyekiti wake, Freeman Mbowe kupokea wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) waliowahi kutuhumiwa na chama hicho.

“Nilitaka kujua iwapo Lowassa atajiunga na CHADEMA ataongeza thamani gani ya chama. Lakini pia yeye mwenyewe atangaze kuachana na Chama Cha Mapinduzi na kisha kujisafisha yeye mwenyewe kashfa zinazomkabili ikiwemo Richmond , masharti haya hayakutekelezwa,” amesema Dk. Slaa na kuongeza

“Mimi sikuwa likizo kama viongozi wangu walivyosema. Niliamua kuachana na siasa kutokana mambo yalivyokuwa ndani ya chama.”

Akizungumza kwa kujiamini Dk. Slaa amesema, hakuona sababu ya kuendelea kutumikia wananchi kupitia chama hicho kwa kuwa, wale aliokuwa akiwatuhumu kwa makosa mbalimbali ikiwemo rushwa na ufisadi sasa wamepokelewa na chama hicho.

Hata hivyo, ametumia muda mwingi kueleza alivyoratibu namna ya kupokea wanachama wapya hasa kutoa CCM huku akiweka vigezo ili kukiweka chama hicho salama kwenye taswira ya wananchi kutokana na misingi yake tangu awali.

Anasema, tangua awali aliweka misingi ndani ya chama hicho kabla ya Lowassa kuhamia chama hicho ikiwa ni pamoja na kutangaza kuachana na chama chake, na nini anakuja nacho kabla ya kumpokea na kwamba “yote haya yalipuuzwa.”

Hata hivyo, Dk. Slaa amesema “sina chuki na mtu yeyote lakini sipendi siasa za udanyanyifu na propaganda. Nimeachana na siasa tangu 28 Julai mwaka huu baada ya kuona misingi ya chama nilichokisimamia na kushiriki kukijenga ikipotoshwa.”

Dk. Slaa amekiri kushiriki vikao ambavyo vilijadili ujio wa Lowassa ndani ya chama hicho lakini amesisitiza kuwa hakukubaliana na uamuzi huo baada ya masharti aliyoyatoa kuhusu Lowassa kujiunga na CHADEMA kupuuzwa.

Pia, amesema baada ya Lowassa kuahidi kwenda CHADEMA na wabunge 50, wenyeviti wa mikoa wa CCM 22 na wenyeviti wa wilaya zaidi ya 80, ahadi hiyo kutotimizwa ni moja kati ya sababu za yeye kujiondoa CHADEMA.

Dk. Slaa amesema, kwa muda wote ndani ya chama hicho, amefanya kazi vizuri na Mbowe na hakuwahi kutofautiana lakini kwa Lowassa wametofautiana.

Tofauti na mikutano mingine aliyowahi kufanywa Dk. Slaa na waandishi wa habari, leo saa 6 mchana tayari waandishi wa habari walifika katika Hoteli ya Serana kulipofanyika mkutano huo ambao ulianza saa 8 mchana.

Katika hali iliyozua mshangao waandishi wa habari hawakuruhusiwa kuingia katika ukumbi wa mkutano mpaka ilipotimu saa 7.30 mchana huku wakiingia kwa vitambulisho.

error: Content is protected !!