August 13, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Dk. Shein, Maalim Seif watikisha Bunge

Spread the love

 

JILA la Maalim Seif Sharif Hamad, Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF) na lile la Dk. Ali Mohammed Shein, Mwenyekiti wa Baraza la Mpainduzi visiwani humo bado yanatikisa bunge, anaandika Faki Sosi.

Ni kutokana na Tume ya Uchaguzi Zanzibar kulazimisha marudio ya uchaguzi uliofanyika tarehe 20 Machi mwaka huu baada ya kufutwa matokeo ya uchaguzi mkuu uliofanyika tarehe 25 Oktoba mwaka jana.

Maalim Seif alikuwa mgombea urais kupitia CUF huku Dk. Shein akiwa mgombea kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM). Kwenye matokeo ya awali katika uchaguzi wa kwanza, Dk. Shein alitajwa kushindwa.

Vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) vimeendelea na msimamo wake wa kulaani uchaguzi haramu uliomrejesha Dk. Shein madarakani na kwamba, ushindi huo ameupoka kutoka kwa Maalim Seif.

Ally Saleh, Waziri Kivuli, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni leo akiwasilisha maoni ya kambi hiyo kuhusu Bajeti ya Ofisi ya Makamu wa Rais-Muungano kwa Mwaka wa Fedha 2016/17 amesema, ushindi wa CCM kwenye uchaguzi wa marudio visiwani Zanzibar ni wa kupika.

Haihitaji  sayansi ya kurusha roketi kujua kuwa matokeo ya Uchaguzi wa Machi 20 huko Zanzibar yalikuwa ni ya kupika,  kuungaunga na kujalizajaliza, kugeuza kura za Maalim Seif na kupewa Dk. Shein na hata kumpa serwa asiyostahiki,  ndio maana urais wake hauna uhalali kwa maana ya misingi ya kidemokrasia,” amesema.

Kwenye hotuba hiyo Saleh amesema, kambi hiyo haioni haja ya kuzungumzia uchaguzi wa marudio kwa kuwa  haukupasa kuwepo.

“Katika huo ulioitwa uchaguzi, Serikali ya Muungano ilipeleka majeshi na silaha Zanzibar ili kuhakikisha kuwa malengo yao ya kuendelea kuitawala Zanzibar kimabavu yapo palepale,” amesema.

Amesema, mpaka sasa Serikali ya CCM imeendelea kuyaweka majeshi yake visiwani humo yakiwa yamevaa mavazi yao ya kijeshi kana kwamba nchi ipo vitani.

“Hivi ninavyozungumza, Zanzibar imetekwa na  Jeshi la Tanganyika. Tangu kipindi cha uchaguzi Mkuu wa kwanza wa Rais na Wawakilishi hadi uchaguzi wa marudio na mpaka sasa majeshi ya JWTZ yapo Zanzibar ‘in full combat’ kana kwamba nchi yetu ipo vitani,” amesema.

Amesema kuwa, kama Jeshi la Tanganyika linatumika kuulazimisha muungano, ni dhahiri kwamba Muungano huo hauna ridhaa ya wananchi na kwa sababu hiyo hautadumu.

“Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inatoa rai kwa serikali hii ya awamu ya tano kwamba; kama kweli ina nia ya kuuenzi na kuudumisha Muungano basi, izingatie maoni ya wanananchi waliyoyatoa kwenye Tume ya Mabadiliko ya Katiba kuhusu muundo wa Muungano ili kuwa na Muungano unaoridhiwa na wananchi wa pande zote mbili za Muungano,” amesema.

Amesema kuwa, viziwani humo kumekuwepo na ukandamizaji wa demokrasia na kwamba, hali hiyo imeanza kujitokeza tangu uchaguzi mkuu wa kwanza wa vyama vingi mwaka 1995.

Amesema, Serikali ya Muungano imekuwa kiini cha uchafuzi wa uchaguzi visiwani humo kwa lengo la kuibeba CCM.

Saleh amesema, “hii bila ya shaka haikuwa mara ya kwanza mikono ya Serikali ya Muungano kuchafuka kutokana na chaguzi za Zanzibar bali imeanza toka katika Uchaguzi Mkuu wa mwanzo wa vyama vingi mwaka 1995.

“… ambapo CUF ilishinda uchaguzi lakini Serikali ya Muungano ikachagua kuibeba CCM Zanzibar na ikawa ni sehemu ya dhulma kubwa kwa Wazanzibari waliotaka mabadiliko mwanzo tu wa kuanzishwa mfumo wa vyama vingi vya siasa.

“Mwalimu Julius Nyerere wakati huo akapendekeza kuundwa serikali ya pamoja lakini akapuuzwa.”

Kwenye hotuba yake amesema, kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni haina haja ya kutaja yaliyotokea katika chaguzi za Zanzibar mwaka 2000 na 2005.

“… lakini itoshe tu kusema kuwa matokeo ya chaguzi zote hizo tatu za mwanzo yalizua  mizozo, migomo, mikwamo, mauaji, ukiukwaji wa haki za binaadamu, ukimbizi wa Wazanzibari, miafaka na hatimaye serikali ya umoja wa kitaifa,” amesema Ally.

Hata hivyo amesema kuwa, Serikali ya Muungano haina nia njema na Muungano huo na kwamba, imefanya hila zote za kuuharibu uchaguzi wa kidemokrasia uliofanyika Zainzibar.

Amesema uchaguzi huo uliipa ushindi CUF lakini Dk. Shein ameunda serikali haramu na kuvunja msingi wa Serikali ya Umoja wa kitaifa uliowekwa na Katiba ya Zanzibar.

Serikali ya Tanganyika inayojidai kwamba ndiyo ya Muungano imesimamia kuvunjwa kwa Katiba ya Zanzibar kwa kuiweka kwa nguvu Serikali haramu huko Zanzibar.

“Nasema hivi kwa sababu, kulikuwa hakuna msingi wowote wa kikatiba wala kisheria wa kufuta uchaguzi wa Zanzibar ambao ulifanyika kwa amani na washindi kutangazwa na kupewa shahada za ushindi.

“Madhila yote hayo yalirudisha nyuma sana maendeleo ya Zanzibar; na Serikali ya hii inayojinasibu kuwa ni ya Muungano ikaridhia hayo yote ilimradi tu CCM Zanzibar ibaki madarakani bila  ridhaa ya wananchi,” amesema Saleh.

Hata hivyo ameikosoa serikali kwamba, imekuwa ikisimamia ama kusemea demokrasia za nchi nyingine wakati ndani ya nchi yake demokrasia hiyo imekuwa ikinyongwa.

Amesema, “wakati tukinyamazia yetu ya ndani Serikali ya Tanzania imekuwa msemaji hodari wa demokrasia za wengine.

“Tumekemea hodari kusemea ukandamizaji wa demokrasia katika nchi nyingine lakini kwetu tunaendelea kujivika “kilemba cha ukoka” kwamba; sisi ni kisiwa cha amani wakati kilichopo ni utawala wa kibabe unaothubutu hata kulifunga bunge mdomo kwa kuamuru vyombo vya habari visitoe habari za bunge live.”

error: Content is protected !!