August 15, 2022

Uhuru hauna Mipaka

‘Dk. Shein haiwezi Z’bar bila CUF’

Spread the love

WAKATI Dk. Ali Mohamed Shein akisubiri kuapishwa kuendelea na wadhifa wake wa urais, imeelezwa kwamba hawezi kuiendesha Zanzibar bila Chama cha Wananchi (CUF), anaandika Faki Sosi.

Kitila Mkumbo, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) amesema, kumalizika kwa uchaguzi wa Zanzibar ambao haukuwepo kisheria, ndio kumeanzisha mgogoro mpya.

Amesema, iwapo Dk. Shein na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kisipotafuta suluhu na CUF, atakuwa kwenye wakati mgumu katika uongozi wake.

“Kumalizika kwa uchaguzi huo ndio kumeanzisha mgogoro mpya Zanzibar,” Mkumbo amesema hayo jana wakati akizungumza na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC Swahili) katika Kipindi cha Dira ya Dunia.

Kitila amefafanua kwamba, kuna Wazanzibari wengi ambao ni wanachama wa CUF na kwamba, chama hicho kikuu cha upinzani kususia uchaguzi huo ikiwa ni pamoja na kutokuwa tayari na matokeo hayo kunaendelea kuzua mgogoro.

Alitoa mfano wa Pemba ambapo zoezi la upigaji kura tarehe 20 Machi mwaka huu lilisuswa kutokana na idadi kubwa ya raia wa kisiwa hicho kuwa wafuasi wa CUF.

“Dk. Shein atalazimika kutafuta njia ya kufaya mazungumzo na CUF na si vinginevyo, katika mazingira haya ni vigumu kuendesha nchi bila CUF.”

Wakati Mkumbo akisema hivyo, Fatuma Karume, Wakili wa Kujitegemea wa Mahakama ya Rufaa jijini Dar es Salaam amesema kwamba, Dk. Shein amewekwa madarakani kinyume na utaratibu wa nchi.

“Kama unawekwa madarakani kwa jeshi, vitisho huwezi kuwa rais wa wananchi,” amesema Fatma ambaye ni mtoto wa Rais Mstaafu wa Zanzibar, Abeid Aman Karume.

Kauli za viongozi wa CUF zinaashiria kujitenga na chochote kitakachofanywa na Dk. Shein kwa madai ya kuwa ni mtawala haramu wa visiwa hivyo.

Kwenye uchaguzi huo CUF iliueleza mtandao huu kwamba, imejiweka kando na utawala wa Dk. Shein kutokana na kubebwa na Jecha Salim Jecha, Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) kwa mapenzi yake binafsi na CCM.

Jecha alifuta matokeo ya Uchaguzi Mkuu uliofanyika visiwani humo tarehe 25 Oktoba mwaka jana kinyume na katiba na pia alitangaza uchaguzi wa tarehe 20 Machi mwaka huu kinyume cha sheria na katiba ya nchi hiyo.

Nassor Ahmed Mazrui, Naibu Katibu Mkuu wa CUF Zanzibar mwishoni mwa wiki aliueleza mtandao huu kwamba wamekaa kimya kuhofia raia wa visiwa hivyo kuuawa kutokana na jeuri ya Serikali ya CCM.

“Dunia ukiiendea mbio mwisho wake ni kuangamia, tunajua dhulma huwa haidumu. Inahitajika sana subra ili kuokoa maisha ya wengi. Tunajua kwamba dhulma imetendeka lakini hakuna shaka hakutakuwa na mwananchi atakayeuawa kwa sababu yetu,” amesema na kuongeza;

‘’Sisi tumetulia, hatuna shaka tunatizama tu watakachoamua kufanya sisi tutakaa kimya kwani hatuko tayari wananchi wetu wamwage damu.”

Hata hivyo Mazrui alisema, “kukaa kimya pia si ujinga, muda ukifika wananchi wataelewa kwa nini tuliamua kujitoa kwenye uchaguzi na kukaa kimya.’’

Magdalena Sakaya, Naibu Katibu Mkuu wa CUF Bara alisisitiza CCM sio mbabe isipokuwa busara na muono wa mbali wa CUF.

“Hakuna marefu yasiyo na nchi,” amesema Sakaya na kuongeza “ wakati wa CCM kuachia nchi unafika, hili halipingiki. Tunajua wananchi hawatuelewi lakini watatuelewa.”

error: Content is protected !!