August 16, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Dk. Shein, Balozi Seif waumbuana

Spread the love

MATOKEO ya kunajisiwa kwa Katiba ya Zanzibar kulikomuweka Dk. Ali Mohammed Shein (CCM) madarakani baada ya uchaguzi wa marudio wa tarehe 20 Machi mwaka huu, yanaanza kudhihiri, anaandika Happiness Lidwino.

Wakati wiki iliyopita Balozi Seif Ali Idd akisema kuwa, Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) ipo pale pale na kwamba, bosi wake Dk. Shein atateuwa wapinzani ili kukabidhi haja ya Katiba ya Zanzibar, rais huyo amesema haiwezekani.

Dk. Shein amesema serikali yake itaundwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) pekee kwa kuwa, hakuna chama kilichofikisha matakwa ya katiba hiyo ili kuunda SUK.

“Balozi Seif Ali Iddi nimemteua kuwa Makamu wa Pili wa Rais kwa mujibu wa sheria na kwa kuwa hakuna nafasi Kikatiba ya kuteua Makamu wa Kwanza wa Rais ama Mawaziri kutoka Upinzani,” amesema.

Dk. Shein mesema hayo katika uzinduzi wa Baraza la Tisa la Wawakilishi Zanzibar uliofanyika leo.

Amesema kwenye uchaguzi wa marudio uliofanyika tarehe 20 Machi mwaka huu, hakuna chama kilichopata kura za rais kwa zaidi ya asilimia 10 isipokuwa CCM, pia hakuna chama kilichopata wabunge isipokuwa CCM.

Wiki iliyopita Balozi Seif Ali Idd ambaye ameteuliwa kuwa Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar alinukuliwa akisema SUK iko palepale.

Balozi Seif alifanya hivyo kwa kujua kwamba, kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar, Dk. Shein hawezi kupata uhalali wa kuendesha serikali bila kuwepo kwa Makamu wa Kwanza wa Rais.

Pamoja na matakwa hayo ya Katiba ya Zanzibar kutaka kuwepo kwa Makamu wa Kwanza wa Rais anayetokana na upinzani ndipo serikali ikamilike, Dk. Shein amepuuza katiba hiyo na kuunda serikali yake nje ya katiba.

Balozi Idd alisema “naamini kuwa Rais (Ali Mohamed) Shein atatumia hekima na busara kuchagua viongozi wa vyama vingine vya upinzani kuendeleza Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) baada ya chama cha CUF kususia uchaguzi,”

Kauli hiyo ilipingwa vikali na Awadh Ali Said, Wakili wa Mahakama Kuu ya Zanzibar ambaye alisema kiongozi huyo kuwa ni mpotoshaji.

Awadh alisema, kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2010 na kuingizwa kipengele cha muundo wa SUK, hakuna hoja itakayohalalisha muundo wa SUK.

“Kwa mujibu wa Katiba na kwa mujibu wa matokeo ya uchaguzi hakuna utata kwa nafasi ya urais na nafasi ya makamu wa pili. Mtihani upo katika kumpata huyu makamu wa kwanza,” alisema Awadh.

Hata hivyo Dk. Shein amedai uchaguzi huo wa marudio nafasi ya rais iligombewa na vyama 14 vya siasa na hakukuwa na chama chochote zaidi ya CCM kilichopata matokeo ya kura za uchaguzi wa rais kwa zaidi ya asilimia 10.

Licha ya Dk. Shein kudai kwamba, uchaguzi huo ngazi ya urais iligombea na vyama 14 kikiwemo Chama cha Wananchi (CUF), viongozi wa CUF walieleza mapema kujitoa kwenye uchaguzi huo waliouitwa ‘haramu’.

Ni baada ya matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa tarehe 25 Oktoba mwaka jana kufutwa na Tume ya Uchaguzi wa Zanzibar (ZEC) kwa madai ya kuwepo na kasoro.

Dk. Shein amesema, kwa kuzingatia msingi huo, na kwa kuzingatia masharti ya kifungu cha 39(3) cha Katiba ya Zanzibar ya 1984, hakuna chama cha siasa ambacho kinakidhi masharti ya kustahiki kutoa Makamu wa Kwanza wa Rais ili kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa.

Amedai vifungu hivyo vya Katiba vinataka Makamu wa Rais ateuliwe ndani ya Balaza la Wawakilishi, atoke katika chama anachotoka rais, na kwamba uteuzi wake umezingatia sheria na Katiba ya Zanzibar.

error: Content is protected !!