July 6, 2022

Uhuru hauna Mipaka

DK. Shein apingwa kushiriki uzinduzi wa Bunge la 11

Spread the love

WAKATI kungali na usiri mkubwa hapa wa vikao vya majadiliano vinavyohusisha viongozi wakubwa wa kisiasa Zanzibar, mpango wa Dk. Ali Mohamed Shein kuomba udhuru ili ashiriki hafla ya uzinduzi wa Bunge la 11 kesho, umelalamikiwa. Anaandika Jabir Idrissa, Zanzibar … (endelea).

Watu mbalimbali wameiambia MwanaHALISI Online leo kuwa hawaridhiki na taarifa kuwa Dk. Shein anaacha majadiliano na kufunga safari ya Dodoma kwa shughuli ambayo inaonekana isiyo umuhimu sana.

Viongozi kadhaa wa vyama vya siasa hapa wamesema hakuna sababu ya msingi Dk. Shein kuondoka Zanzibar wakati hata huo uhalali wa urais wake unatiliwa shaka kwa kuwa ameshatimiza kipindi chake cha miaka mitano tangu kuapishwa Novemba 2 mwaka 2010.

Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, Ibara ya 28(2) inasema rais atakaa madarakani kwa kipindi cha miaka mitano kutoka tarehe ile aliyokula kiapo cha uaminifu na kiapo cha kuwa rais wa Zanzibar.

Wanasheria wanashikilia kuwa kipindi cha urais cha Dk. Shein kilimalizika Novemba 2 mwaka huu na kwamba alitakiwa kuondoka madarakani.

Wasaidizi wa Dk. Shein wanasema rais huyo bado ni halali mpaka pale atakapoapishwa rais mwingine. Hoja yao wanaitoa kwa kutumia Ibara hiyohiyo ya 28, kifungu cha kwanza.

Dk. Shein amebakia katika hali hiyo ya utata wa uhalali wake kutokana na Zanzibar kutopata rais mpya kufuatia uamuzi wa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar, Jecha Salim Jecha kufuta uchaguzi wa Oktoba 25 kwa madai kuwa uliharibika.

Uamuzi huo alioutoa Oktoba 28 mwaka huu, umesababisha matatizo ya kukwama kwa uchaguzi kwa vile matokeo hayakuendelea kutangazwa tena, wakati mpaka hapo Jecha mwenyewe alikuwa ameshatangaza matokeo ya kura za urais za majimbo 31, yote yakiwa ya kisiwani Unguja.

Zanzibar ina majimbo 54 ya uchaguzi yakiwemo 18 ya kisiwani Pemba. Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimepata viti 27 vya uwakilishi, sawa na ilivyopata Chama cha Wananchi (CUF).

error: Content is protected !!