August 10, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Dk. Shein ajitetea

Spread the love

DK. Ali Mohamed Shein, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi visiwani humo amejitetea kwamba ushindi wake ni halali, anaandika Regina Mkonde.

Akizungumza kwenye Maadhimisho ya Siku ya Mashujaa iliyofanyika Dodoma jana, Dk. Shein amesema wapo wanaolalamikia ushindi wake na kwamba, licha ya malalamiko hayo ataendelea kufanya kazi kwa amani na Rais John Magufuli.

Hata hivyo amepiga kijembe kwamba, kelele za mlangoni hazimzuii mwenye nyumba kulala. Ingawa hakutaja moja kwa moja jina la Maalim Seif Sharif Hamad lakini bila shaka kauli hiyo inamlenga yeye (Maalim Seif) ambaye amekuwa akilalamikia kupokwa ushindi wake na kiongozi huyo wa CCM.

Safari za kutafuta haki nje ya nchi za Maalim Seif, Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF) pia aliyekuwa mgombea urais visiwani humo katika uchaguzi mkuu wa mwaka jana zinaonekana kuitia kiwewe CCM Zanzibar.

CCM visiwani Zanzibar imekuwa ikitoa matamko makali ikiwa ni pamoja na kutaka Maalim Seif akamatwe kwa madai ya kufanya uchochezi.

Baada ya kufutwa matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana na kurudiwa tarehe 20 Machi mwaka huu, Maalim Seif amekuwa akiilalamikia Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) kupoka ushindi wake na kumtunuku Dk. Shein.

Ndani ya nchi na katika jumuiya za kimataifa Maalim Seif amekuwa akitaka Serikali ya Dk. Shein isipewe ushirikiano wowote kwa madai ya kunyonga demokrasia.

Hata hivyo, zaidi ya mara moja Maalim Seif amekuwa akisema yeye ndiye mshindi na kwamba Wazanzibari wanatambua hivyo.

Pia amekuwa akisema ataendelea kudai haki yake ya ushindi wa uchaguzi mkuu wa tarehe 20 Oktoba mwaka jana kwa njia ya amani.

error: Content is protected !!