July 1, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Dk. Shein, Maalim Seif wateta

Spread the love

WANASIASA wawili wanaogombania kutwaa urais katika uchaguzi mkuu wa Zanzibar wa Oktoba 25, walikutana mjini hapa jana na kuamsha upya “imani” miongoni mwa wananchi kwa vile huo ni mkutano wa kwanza kwao tangu uchaguzi huo ulipofutwa kinyemela Oktoba 28, mwaka huu. Anaandika Jabir Idrissa, Zanzibar … (endelea0.

Dk. Ali Mohamed Shein aliyegombea tena urais kwa tiketi ya Chama Cha Maponduzi (CCM), na Makamu wake wa Kwanza wa Rais, Maalim Seif Sharrif Hamad, aliyegombea kwa mara ya tano mfululizo, walikutana Ikulu ya Zanzibar.

Hakuna upande wowote kati ya viongozi hao uliotoa maelezo baada ya kukutana kwao, ingawa vyanzo vya ndani ya serikali, Chama Cha Mapinduzi na Chama cha Wananchi (CUF), vimethibitisha mazungumzo ya viongozi hao yalichukua karibu saa nne kumalizika.

Mwandishi wa habari hizi alipata taarifa awali kuwa ratiba ya kikao cha viongozi hao ilikuwa kuanzia saa 4 asubuhi hiyo jana, lakini inasemekana kilichelewa kidogo kuanza. Lakini, hakuna sababu iliyoelezwa ya ucheleweshaji huo na ni nani hasa alisababisha.

Katika hatua nyingine, imeelezwa kwamba kikao cha viongozi hao, pia kilimshirikisha Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi, ambaye mwenyewe aligombea kiti cha uwakilishi, jimbo jipya la Mahonda, Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Taarifa zaidi zimesema kwamba marais wawili wastaafu wa Zanzibar, Ali Hassan Mwinyi aliyeongoza mwaka mmoja tu kufikia mwaka 1985 alipohamishiwa Tanzania Bara na kuchaguliwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na Amani Abeid Amani Karume, aliyeingia Ikulu Novemba 2000 na kutoka Novemba 2010 baada ya kufanikisha mkataba wa kihistoria wa maridhiano na Maalim Seif uliowezesha kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) baada ya uchaguzi mkuu.

Haifahamiki ni katika mazingira gani aliitwa Mzee Mwinyi lakini akaachwa Dk. Salmin Amour Juma ambaye aliongoza vipindi viwili kufikia 2000 ulipofanyika uchaguzi mkuu.

Maofisa wa Ikulu ya Zanzibar hawakuwa tayari kueleza undani wa kikao cha viongozi hao, lakini wale wa CUF walithibitisha kuwa majadiliano yalikuwa “ni mema kwa maslahi ya nchi.”

Zipo taarifa kwamba ni Maalim Seif aliyetaka Mzee Mwinyi ashiriki kikao hicho, lakini hakuna aliyethibitisha taarifa hizo, na wala haikuelezwa sababu ya kualikwa kiongozi mstaafu huyo ambaye kwa Wazanzibari wapenda mabadiliko, anaonekana kama “adui” wa maendeleo ya Zanzibar.

Tangu kustaafu uongozi mwaka 2000, Dk. Salmin amekuwa haonekani mara kwa mara hadharani kutokana na hali yake ya afya. Hata kabla ya kustaafu, alipata upofu wa macho, na mara ya mwisho alipokutana na waandishi wa habari nyumbani kwake Migombani, mjini haopa, alisema, “sasa hivi angalau naweza kusoma magazeti, sijambo alhamdulillahi.”

Hata hivyo, hali yake ilionekana wazi kuwa macho yake hayakuwa na uwezo tena wa kusoma chochote, na kwa jumla kuona.

Ingawa hakuna maelezo ya undani wa mazungumzo yalivyokuwa, kule kukutana kwa Dk. Shein na Maalim Seif wakati huu, kunaweza kurudisha imani kwamba utatuzi wa mgogoro uko nchani kupatikana.

Kikao kilichowakutanisha Dk. Shein na makamu wake wawili kimefanyika ndani ya hali isiyoeleweka kwa sasa, kwa vile nchi imeganda baada ya kuingizwa kwenye mgogoro wa uchaguzi mkuu.

Mgogoro huo umetokana na hatua ya Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha, kutangaza uamuzi wa “peke yake” wa kufuta uchaguzi wote nchi nzima huku akiwa ameshatangaza matokeo ya urais kwa majimbo 31 kati ya 54 yote ya Zanzibar.

Uamuzi huo unatambuliwa kuwa ni wa peke yake, kwa sababu umethibitishwa kutokana na majadiliano ya ndani ya Tume hiyo, na kwa kuwa si yeye mwenyekiti wala Tume, yenye mamlaka ya kisheria ya kufanya hivyo.

Hakuna kifungu cha sheria katika Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar, Na. 11 ya mwaka 1984, wala katika Katiba ya Zanzibar ya Mwaka 1984, kinachotoa mamlaka hayo kwa namna yoyote ile.

Hii imethibitishwa na tamko lake mwenyewe Jecha ambalo pamoja na kuwa alilisaini, hakueleza amepewa mamlaka hayo na kifungu gani cha sheria.

Jecha alitangaza uamuzi huo Oktoba 28, siku ya pili, makamishna wawili wa Tume hiyo kutoka CUF, Nassor Khamis Mohamed, na Ayub Bakari, walimkana wakieleza kuwa alichokifanya si halali kwani hakuna mamlaka yaliyompa nguvu, na hakuna kikao cha Tume kilichofanyika hata kufikia uamuzi wa kumtuma kufanya hivyo.

Aidha, Jecha alitoa tangazo hilo siku mbili baada ya Maalim Seif kueleza kwamba mwelekeo wa kura ulikuwa wa kumpatia ushindi wa asilimia 52.87 dhidi ya asilimia 47.13 za Dk. Shein.

Maalim Seif aliyetoa taarifa hiyo mbele ya waandishi wa habari, kwenye makao makuu ya CUF, alisema alitarajia Tume itangaze matokeo pasina kuchelewesha na kumtaka Dk. Shein akubali amepoteza mamlaka na kutangaza rasmi kama alivyofanya yeye mwaka 2010.

Kukutana kwa viongozi hao kunachukuliwa kama hatua muhimu katika kurudisha “wanasiasa wahafidhina wa CCM” katika ufahamu wao wa akili kwa vile dunia inauhakika kuwa wao ndio tatizo.

Matokeo ya uchaguzi yalikuwa tayari yamesainiwa na wasimamizi wa vituo vya uchaguzi nchi nzima katika majimbo yote 54, na hata wakala mkuu wa Dk. Shein, Balozi Mohamed Ramiya Abdiwawa, alisharidhia na ikaelezwa “aliharakia kumpa taarifa ya kushindwa Dk. Shein.”

“Ukweli Dk. Shein ameingizwa tu katika mgogoro ili aonekane tatizo, lakini aliharakia kukubali kushindwa na kusema, ‘siwezi kubadilisha uamuzi wa wananchi.”

Viongozi wanaotajwa kuchimba mgogoro ni wale watatu walioonekana kwenye vyombo vya habari Oktoba 29, wakitoa malalamiko kuwa CCM ilihujumiwa.

Hao ni Spika Pandu Ameir Kificho,Waziri Kiongozi mstaafu Shamsi Vuai Nahodha na Naibu Katibu Mkuu wa CCM, Vuai Ali Vuai ambao duru ndani ya CCM zinasema wanaungwa mkono na Balozi Seif.

error: Content is protected !!