RAIS Dk. Samia Suluhu Hassan, ameagiza fedha kiasi cha Sh. 960 milioni, zilizotengwa kwa ajili ya maadhimisho ya miaka 61 ya uhuru wa Tanzania Bara yaliyotarajiwa kufanyika kitaifa 2022, kwenda kujenga mabweni katika shule nane za msingi za watu wenye mahitaji maalum. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).
Uamuzi huo umetangazwa leo Jumatatu, tarehe 5 Desemba 2022 na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), George Simbachawene, akizungumza na wanahabari kuhusu maandalizi ya maazimisho hayo, jijini Dodoma.
Simbachawene amesema, Rais Samia amechukua uamuzi huo ili kuhakikisha kwamba fedha zilizopangwa kutumika kuadhimisha miaka 61 ya uhuru, zinaleta tija kwa jamii.
Amesema tayari fedha hizo zimeshapelekwa katika Wizara ya Ofisi ya Rais-TAMISEMI, kwa ajili ya utekelezaji.
“Hivyo sherehe za mwaka huu hakutakuwa na gwaride wala shughuli nyingine za kitaifa ambazo zitafanyika kwenye uwanja au mahala pamoja,” amesema Simbachawene.
Ametaja shule za wanafunzi wenye mahitaji maalum zitakazonufaika kuwa ni, Buhangija iliyoko Shinyanga, Goweko (Tabora), Darajani (Singida), Mtanga (Lindi), Songambele (Manyara), Msanzi (Rukwa), Idofi (Njombe) na Longido (Arusha).
Aidha, Simbachawene amesema sherehe za maadhimisho hayo yenye kauli mbiu ya “miaka 61 ya uhuru, amani na umoja ni nguzo ya maendeleo yetu”, yatafanyika kupitia makongamano mbalimbali yatakayofanyika katika mikoa na wilaya za Tanzania Bara.
“Makongamano yatatumika kujadili, kutafakari na kukumbuka tulipotoka, tulipo na tunapoelekea kuhusu maendeleo endelevu ambayo nchi yetu imeyapitia na kuyafikia. Kufanya shughuli za kijamii ikiwemo kufanya usafi maeneo ya kijamii, hospitali, nyumba za wazee na makundi maalum,” amesema Simbachawene.
Leave a comment