August 13, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Dk. Rutengwe alalamikiwa ‘kutesa’

Spread the love

WAKAZI wa Mtaa wa Mjimpya Kata ya Saranga, Kinondoni, Dar es Salaam wamemlalamikia Dk. Rajab Rutengwe, aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro kwa kuwapa mateso, anaandika Aisha Amran.

Wakazi hao wamedai kukosa kufikia huduma za kijamii kwa wakati kutokana na Dk. Rutengwe kuziba njia ambayo walikuwa wakiitumia.

Kwa zaidi ya miaka minne sasa wakazi hao wameeleza kumwomba njia ambayo ingewawezesha kufikia huduma za kijamii kwa haraka lakini wamekwama.

Catherine Mushi, mkazi jirani wa Dk. Rutengwe amesema, walimwandikia barua ili waweze kutatua mgogoro huo lakini hakutekeleza ambapo alidai amebanwa na majukumu ya kikazi na kuomba afuatwe Morogoro.

“Tulimwandikia barua ya kumwita kuja kuona jinsi alivyoweka uzio wake vibaya ambao angalau kisheria alipaswa kuacha mita moja na nusu jambo ambalo hakufanya,” amesema Catherine.

Amesema licha ya jitihada ya kumwandikia barua na kumwomba njia zaidi ya miaka minne tangu aweke uzio katika eneo hilo, mpaka sasa hajafanya chochote.

Daniel Maginge, Mwenyekiti wa Kata ya Saranga amuethibitishia mtandao huu kuwa, walimfuata Dk. Rutengwe hadi Morogoro na kumweleza kuhusu malalamiko ya kuomba mita moja na nusu kwa ajili ya njia.

Anasema majibu ya Dk. Rutengwa yalikuwa ni “mpaka aongee na familia yake kwanza ndio atatoa majibu.”

Amesema, “tunafanya jitihada nyingine za kumtafuta ili tuweze kuzungumza nae tujue ana muafaka gani wa kuwasaidia wakazi wa eneo hilo ili waweze kufikia huduma za kijamii kwa urahisi.

“Kuna familia zaidi ya 20 zinaathirika kwa sababu ya uamuzi wa Rutengwe, kimsingi alitumia vibaya madaraka yake kutunyanyasa.”

Waandishi wa MwanaHALISI wamefika kwenye eneo hilo na kushuhudia umuhimu wa kuwepo kwa njia hiyo.

“Tunapata shida sana, inapofika wakati wa kujifungua au kuleta mizigo mingine kwenye eneo letu, tunategemea kudra za Mungu, kweli huyu baba hana huruma na binadamu wenzake,” amesema Khadija Hussein, mkazi wa eneo hilo.

Mtandao huu umemtafuta Dk. Rutengwe ili kujibu tuhuma hizo ambapo kila mara alipopigiwa simu, hakupokea, na alipotumiwa ujumbe mfupi wa maneno, hakuujibu.

“Mheshimiwa Rutengwe, Salama? Hapa ni MwanaHALISI, kuna wananchi wa mjimpya, Kata ya Saranga wanakulalamikia kwamba umejenga uzio hadi kuzuia njia na hawapati huduma muhimu za kijamii. Je, ukweli wa jambo hili ukoje?” ujumbe huo ndio uliotumwa kwake ambapo mpaka habari hii inaandika, hakuujibiwa.

error: Content is protected !!