June 17, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Dk. Possi: Riba nafuu zitasaidiwa wasiojiweza

Spread the love

TAASISI za kifedha nchini zimetakiwa kutoa mikopo yenye riba nafuu kwa watu waishio maeneo ya vijijini hususan makundi ya watu wasiojiweza ikiwemo walemavu wa viungo ili waondokane na hali ya utegemezi, anaandika Regina Mkonde.

Hayo yamesemwa leo na Dk. Abdallah Possi, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Watu Wenye Ulemavu wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam baada ya kufungua mkutano wa mpango unaohusisha masuala ya fedha maeneo ya vijijini.

“Taaasisi ndogondogo za kifedha na benki, zitambue kwamba watu wa vijijini hawana mitaji mikubwa, na kwamba zikiwepo taasisi za ikfedha zinazolenga kutoa huduma shirikishi vijijini, zitawafikia na kusaidia wengi,” amesema na kuongeza.

“Wengi watapata fursa ya kujiendeleza kiuchumi kupitia kilimo,  watawekeza kwenye ufugaji kwa maana hiyo vijijini hakutakuwa tena sehemu ya kutengwa kama watu wanavyodhani hakuna maisha mazuri.”

Amesema huduma hizo zitabadilisha mtazamamo kwa kuwa kule vijijini ndiyo kuna wakulima, kuna wafugaji kwa hiyo waitutumie fursa hiyo kutoa huduma za msingi na sahihi.

Aidha, amesema kuwa mikopo hiyo itakapowafikia walemavu itawasaidia kujikwamua kiuchumi.

“Tuna kundi ambalo kulingana na tamaduni potofu na masuala mengine mbalimbali limekuwa likiachwa nyuma kwa muda mrefu, na kupelekea kukosa msaada wa kujikwamua kiuchumi,” amesema na kuongeza.

“Mwenye ulemavu akipata huduma ya kifedha, ikiwemo mikopo anaweza akajitegemea na kuibadilisha dhana ya walemavu kuwa tegemezi na badala yake watakuwa wadau wa uzalishaji na maendeleo,” amesema.

Joel Mwakitalu, Mwenyekiti wa Shirikisho la Taasisi za Fedha nchini, amesema kuwa awali taasisi a kifedha zilikuwa zinashindwa kupeleka huduma za kifedha vijijini kutokana na changamoto ikiwemo ya miundombinu.

“Changamoto zinazotukabili katika kufikisha huduma vijijini ni miundombinu,  labda changamoto hii itarahisishwa na huduma za simu, licha ya hivyo kuna sehemu watu hawafikiwi na simu, hivyo bado kuna changamoto,” amesema.

 

error: Content is protected !!