RAIS Mteule wa Zanzibar, Dk. Hussein Mwinyi anatarajiwa kuapishwa Jumatatu ijayo ya tarehe 2 Novemba 2020, katika Viwanja vya Amani visiwani humo. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).
Taarifa hiyo imetolewa leo tarehe 31 Oktoba 2020 na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Humphrey Polepole wakati anazungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam.
“Ningependa kusisitiza siku ya Jumatatu kule Zanzibar Wazanzibar wote na Watanzania wote wenye mapenzi mema na demokrasia wajitokeze kwa wingi Viwanja vya Amani ambapo ndugu yetu ataaapishwa kuwa rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar awamu ya nane. Hivyo shime Watanzania wote mjitokeze kwenda kushuhudia tukio hilo,” amesema Polepole.
Dk. Mwinyi aliyekuwa Mgombea Urais wa Zanzibar kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika tarehe 28 Oktoba 2020, alishinda kiti hicho kwa kupata asilimia 76.27 ya kura huku aliyekuwa mpinzani wake karibu kupitia ACT-Wazalendo, Maalim Seif sharif Hamad akipata asilimia 19.87.

Polepole amesema sherehe hiyo ya uapisho itaongozwa na Rais Mteule, Dk. John Magufuli na Rais wa Zanzibar anayemaliza muda wake, Dk. Ali Shein.
Wakati Dk. Mwinyi akitarajia kuapishwa siku ya Jumatatu ijayo, Dk. Magufuli anatarajia kuapishwa tarehe 5 Novemba 2020 katika Viwanja vya Jamhuri jijini Dodoma.
“Tarehe 5 Novemba 2020 katika viwanja vya Jamhuri Dodoma taarifa inatolewa kwa Watanzania wote kutafanyika tukio lingine kubwa la kihistoria ambapo ndugu yetu John Magufuli ataapishwa kule Dodoma. Shime karibuni sana viwanja vya Jamhuri tukashuhudie uongozi wa kidemokrasia Tanzania,” amesema Polepole.

Jana tarehe 30 Oktoba 2020 Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ilimtangaza Dk. Magufuli aliyekuwa mgombea urais wa Tanzania wa CCM kushinda uchaguzi huo baada ya kupata kura milioni 12.5 kati ya milioni 15.9 zilizopigwa, wakati aliyekuwa mpinzani wake kupitia chama cha Chadema, Tundu Lissu akipata kura milioni 1.9.
Leave a comment