May 21, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Dk. Mwinyi awakumbusha wajibu wao wateule wake

Spread the love

 

RAIS wa Zanzibar, Hussein Mwinyi amewasisitiza viongozi aliowateua kwenda kwa wananchi kuwasikiliza changamoto walizonazo na kuyatafutia ufumbuzi. Anaripoti Mwandishi Wetu, Zanzibar … (endelea).

Rais Mwinyi ameyasema hayo wakati akitoa salamu kwa wananchi wa kijiji cha Nungwi baada ya sala ya Ijumaa leo tarehe 29 Januari 2021, katika Masjid Rahman iliyopo Nungwi, Wilaya ya Kaskazini A, Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Katika salamu zake, Rais Mwinyi amesema, kuna kila sababu kwa viongozi wake wakiwemo wakuu wa wilaya na mikoa kwenda kuwasikiliza wananchi changamoto zao ili ziweze kupatiwa ufumbuzi.

Amesema, amegombea nafasi ya Urais kwa ajili ya kuwatumikia wananchi kwa kuwasikiliza matatizo yao, kero zao zikiwemo huduma za jamii kama vile afya, elimu, maji na nyenginezo ambapo hivi sasa amekuwa akifanya mikutano kadhaa na wadau wa sekta hizo kwa azma ya kutatua changamoto zilizopo.

Rais Mwinyi amesema, changamoto hizo zinashughulikiwa na kusisitiza tayari alishawaambia wateule wake wakati akiwaapisha washuke chini wakawashughulikie wananchi changamoto zao za ardhi, kuondoa dhulma na changamoto nyenginezo.

Amewapa maagizo Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja na Mkuu wa Wilaya Kaskazini A, wakutane na uongozi kwa ajili ya kusikiliza changamoto za wananchi wa kijiji cha Nungwi na kuwataka wakatatue na yale yaliyo chini ya uwezo wao wamjuulishe ili ayafanyie utatuzi.

Rais Mwinyi amesema, ana dhima ya kuhakikisha ana tenda haki kwa wananchi wote bila ya kujali uwezo wao kifedha, itikadi zao za kisiasa kwani yeye ni Rais wa Zanzibar na ana wajibu wa kuwatumikia wananchi wote bila ya kujali matabaka, rangi, dini wala kabila.

error: Content is protected !!