May 21, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Dk. Mwinyi atumia mbinu ya JPM kuwabana mafisadi Z’bar

Dk. HUssein Mwinyi, Rais wa Zanzibar

Spread the love

 

HATUA iliyochukuliwa na Rais John Magufuli kuanzisha Mahakama ya Mafisadi mwaka 2016, mahakama hiyo sasa inaanzishwa visiwani Zanzibar. Anaripoti Mwandishi Wetu, Zanzibar … (endelea).

Rais Magufuli alitoa ahadi ya kuanzisha mahakama hiyo kwenye mikoa kadhaa aliyopita wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu mwaka 2015.

Tamko la kuanza kazi kwa mahakama hiyo lilitolewa tarehe 22 Aprili 2016, bungeni na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati akiwasilisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya ofisi yake kwa mwaka 2016/17.

“Kuhusu ahadi ya kuanzisha Mahakama Maalum ya Ufisadi, napenda kuliarifu Bunge lako kwamba, serikali imeanzisha Divisheni ya Mahakama ya Rushwa na Ufisadi katika Mahakama Kuu itakayoanza kufanya kazi mwezi Julai 2016,” alisema Majaliwa.

Hatua ya uanzishwaji wa mahakama hiyo, imeanza Zanzibar ambapo rais wa nchi hiyo, Dk. Hussein Mwinyi ameiagiza mahama kuanzisha ‘Mahakama ya Mafisadi’ kwa ajili ya kesi za uhujumu uchumi na rushwa.

Akizunguza wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Sheria visiwani humo tarehe 8 Februari 2021, Dk. Mwinyi amesema, mahakama hiyo inahitajika.

“Jaji Mkuu alisema hapa huenda tutahitaji mahakama maalumu ya rushwa na uhujumu uchumi, mimi nasema sio huenda, hii inahitajika,” alisema Dk. Mwinyi.

Rais John Magufuli

Rais huyo wa Zanzibar amesema, serikali yake imejipambanua kukabiliana na watendaji wanaotumia vibaya madaraka waliyopewa, lakini pia wale wanaojiusisha na wizi na ubadhirifu wa mali ya umma.

Amesema, ndio maana alichukua hatua ya kuwasimamisha kazi watendaji walitajwa kuhusika katika ubadhirifu wa mali za umma ikiwa ni baada ya kupokea ripoti ya tuhuma hizo kutoka kwa Mamlaka ya Kupambana na Rushwa na Uhujumu wa Uchumi Zanzibar (Zaeca).

Kwenye maadhimisho hayo, Dk. Mwinyi alieleza kufurahishwa na mahakama baada ya kutekeleza agizo lake alilolitoa tarehe 7 Januari 2021, la kuanzishwa Mahakama Maaalumu ya Udhalilishaji.

“Na mimi basi tayari nimesharidhia kuajiriwa kwa mahakimu zaidi kama ilivyoombwa,” alisema huku kisisitiza uharaka wa usikilizaji wa mashauri mahakamani na kutoa hukumu kwa wakati.

error: Content is protected !!