May 20, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Dk. Mwinyi akwepa kumzungumzia Maalim Seif

Spread the love

 

RAIS wa Zanzibar, Dk. Hussein Mwinyi amekwepa kuzungumzia hali ya makamu wake wa kwanza, Maalim Seif Sharif Hamad. Anaripoti Mwandishi Wetu, Zanzibar … (endelea).

Akizungumza na wanahabari jana tarehe 9 Februari 2021 visiwani humo, Dk. Mwinyi alisema, hawezi kuzungumzia maendeleo ya ugonjwa wa Maalim Seif hilo kwa kuwa ni kinyume na maadili ya kidaktari.

Rais Mwinyi, alikuwa akizungumza na wanahabari, kuhusu siku 100 za utawala wake, tangu alipoingia madarakani tarehe 2 Novemba 2020, akipokea kijiti kutoka kwa Dk. Ali Mohamed Shein, aliyemaliza muda wake wa uongozi.

“Kuhusu hali ya afya ya makamu wa kwanza wa rais, niseme mimi ni daktari, maadili hayataki kuzungumzia ugonjwa wa watu hadharani,” alisema Dk. Mwinyi.

Alitoa kauli hiyo alipoulizwa na wanahabari kuhusu hali ya Maalim Seif, baada ya chama chake kutoa taarifa za ugonjwa wake kwa umma.

“Kama kuna watu wanasema hivi wanakosea, hali ya ugonjwa wa mtu ni siri yake na daktari. Sio sababu mimi daktari, lakini madili hayako hivyo labda wazungumze wenyewe,” alisema Dk. Mwinyi.

Taarifa za awali zinaeleza, kwamba Maalim Seif anaendelea na matibabu katika Hospitali ya Mnazi Mmoja, Unguja visiwani humo.

Maalim Seif alilazwa hospitalini hapo tangu tarehe 26 Januari 2021, baada ya kuthibitika kuwa na maambukizi ya Virusi vya Corona (Covid-19).

Maalim Seif Sharrif Hamad, Makamu wa Kwanza wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar

Akizungumza na MwanaHALISI Online kuhusu hali ya Maalim Seif, leo Jumatano tarehe 10 Februari 2021, Ado Shaibu ambaye ni Katibu Mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo, amesema anaendelea vizuri.

Amesema, kwa sasa wanamuombea kwa Mungu Mwenyekiti huyo wa Chama cha ACT-Wazalendo, apone haraka ili arejee katika majukumu yake.

“Hali ya Maalim Seif nashukuru Mungu anaendelea vizuri, afya yake ina-improve (inaimarika). Tunamuombea kwa Mungu apone, arejee kwenye majukumu yake. Kwa uelewa wangu hadi jana anaendelea na matibabu,” amesema Ado.

error: Content is protected !!