December 3, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Dk. Mwinyi aeleza sababu kumwangukia Maalim Seif

Dk. Hussein Ali Mwinyi, Rais wa Zanzibar

Spread the love

RAIS wa Zanzibar, Hussein Mwinyi amesema, aliamua kufanya mazungumzo na Chama cha ACT-Wazalendo kinachoongozwa na Maalim Seif Shariff Hamad ili kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUKI), kwa lengo la kupona majeraha ya kisiasa visiwani humo. Anaripoti Mwandishi Wetu, Pemba…(endelea).

Amesema, licha ya ukweli kwamba baadhi ya watu ndani ya chama chake – Chama Cha Mapinduzi (CCM) na ACT-Wazalendo hawaoni sababu za SUKI, amewataka kuvuta subira na kuwa manufaa yake watayaona.

Akizungumza na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Pemba katika ziara yake ya kuwashukuru leo Ijumaa tarehe 18 Desemba 2020, Rais Mwinyi amekumbushia hali mbaya ya mahusiano ya wakazi wa visiwa hivyo viwili (Unguja na Pemba) ilivyokuwa.

“Ndugu zangu WanaCCM, natambua fika kwamba tupo baadhi yetu ndani ya CCM na natambua vilevile wako baadhi ndani ya vyama vya upinzani ambao hawajafurahia hili suala la Serikali ya Umoja wa Kitaifa, lakini ombi langu tuendelee kupeana elimu,” amesema Rais Mwinyi

“Leo ndani ya nchi moja tulifika hatua ya kugawana mpaka Misikiti, watu tulikuwa hatuzikani, wanagombana mke na mume, talaka zilikuwa nyingi. Sisi tunasema hayo sasa tuyaweke nyuma yetu tutengeneze umoja.”

Rais huyo na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Visiwani humo, amewataka kuendelea kuelimishana juu ya umuhimu wa umoja na ushirikiano na kwamba, isingekuwa rahisi kupiga hatua za maendeleo iwapo Zanzibar ingebaki vipande.

“Baadaye hata wale wanaosita sita wataona umuhimu wake, kwa sababu katika hali hii tuliyokuwa nayo ya umoja, amani na ushirikiano, maendeleo yatakuwa makubwa,” amesema Dk. Mwinyi.

Chama cha ACT-Wazalendo kilisuasua kutekeleza takwa la Katiba ya Zanzibar la uundwaji wa SUKI, kutokana na dosari zilizojitokeza katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika tarehe 27 na 28 Oktoba 2020.

Maalim Seif Sharrif Hamad, Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo

Chama hicho pamoja na vyama vya upinzani kadhaa, vilisusa kushirikiana na Serikali ya CCM vikipinga matokeo ya uchaguzi huo, kwa madai mchakato wake haukuwa huru na wa haki.

Baada ya kuapishwa kuwa Rais wa Zanzibar, Mwinyi alimuandikia barua Maalim Seif, aliyegombea urais visiwani humo kupitia ACT-Wazalendo, akimuomba ushirikiano wake katika kuunda serikali hiyo.

Wiki mbili baadaye, ACT-Wazalendo kupitia kikao cha Kamati Kuu yake kilichofanyika tarehe 5 Desemba 2020 jijini Dar es Salaam, iliridhia ombi la Dk. Mwinyi la uundwaji wa SUKI na siku hiyohiyo, Rais Mwinyi alimmteua Maalim Seif kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar.

Akizungumzia ushirikiano huo, Rais Mwinyi amesema, wamekubaliana kuweka tofauti zao pembeni na kwamba wanashirikiana kwa pamoja kwa ajili ya maslahi ya Wazanzibari.

Rais huyo aliyegombea kupitia CCM, alitangazwa na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) mshindi wa urais visiwani humo kwa kupata asilimia 76.27 huku Maalim Seif, aliyekuwa mgombea wa ACT-Wazalendo akipata asilimia 19 ya kura zilizopigwa.

error: Content is protected !!