JAJI Mkuu wa Zanzibar, Othuman Ali Makungu amemuapisha Dk. Hussein Ali Mwinyi kuwa Rais wa Zanzibar. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Dk. Mwinyi (53) ameapishwa leo Jumatatu tarehe 2 Novemba 2020 katika Uwanja wa Aman akichukua nafasi iliyoachwa wazi na Dk. Ali Mohamed Shein ambaye amemaliza muda wake wa uongozi wa miaka kumi kwa mujibu wa Katiba.
Shughuli hiyo imehudhuliwa viongozi mbalimbali wa wa ndani na nje ya Zanzibar wakiwemo marais wastaafu wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete na Ali Hussen Mwinyi.
Pia, Rais mstaafu wa Zanzibar, Aman Abeid Karume, Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa na Makamu wa Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan pamoja na mawaziri wa serikali za Tanzania na Zanzibar.
Dk. Mwinyi aliwasili uwanjani hapo saa 4:04 asubuhi akitumia magari ya kawaida na baada ya kushuka kwenye gari, Jaji Makungu aliongoza msafara kwenda jukwaa maalum la kiapo.
Msafara wa Rais anayemaliza muda wake uliingia kisha alikwenda eneo maalum lililokuwa limeandaliwa kwa ajili ya wimbo wa Zanzibar na mizinga 21 ilipigwa.
Kisha, gwaride la vikosi vya ulinzi na usalama, vilichora umbo la alfa na omega kuashiria mwanzo na mwisho wa utawala wa Dk. Shein ambalo alilikagua.
Baada ya kumaliza kulikagua, ulipigwa wimbo maalum wa kuashiria ukomo wa utawala wa Dk. Shein ikiwa ni saa 4:33 asubuhi ambapo bendera ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ilishushwa.
Baada ya hatua hiyo, Rais Shein alikwenda jukwaa lililokuwa limeandaliwa kwa kiapo ambapo Dk. Mwinyi aliapishwa na Jaji Makungu ikiwa ni saa 4:52 kuwa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Rais Mwinyi, baada ya kuapishwa, alikwenda eneo lililokuwa limeandaliwa ambapo aliimbiwa wimbo wa Taifa na baadaye bendera ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar iliyokuwa imeshushwa ikapandishwa kuashiria mwanzo wa utawala wake.
Rais Mwinyi ambaye ni mtoto wa Rais mstaafu wa visiwa hivyo na wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ali Hussein Mwinyi, anakuwa Rais wa nane wa Zanzibar tangu mapinduzi ya Zanzibar yaliyofanyika tarehe 12 Januari 1964.
Marais wengine walimtangulia na miaka yao kwenye mabano wa kwanza ni; Abeid Karume (26 Aprili 1964- 7 Aprili 1972), Aboud Jumbe (7 Aprili 1972- 30 Januari 1984), Ali Hassan Mwinyi (30 Januari 1984- 24 Oktoba 1984), Idris Abdul Wakil (24 Oktoba 1985- 25 Oktoba 1990).
Salmin Amour (25 Oktoba 1990- 8 Novemba 2000), Aman Abeid Karume (8 Novemba 2000- 3 Novemba 2010) na Dk. Ali Mamohed Shein aliingia 3 Novemba 2010 hadi leo Jumatatu anapokabidhi madaraka kwa Dk. Mwinyi.
Leave a comment