August 19, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Dk. Mwigulu, Bashungwa wawekwa kikaangoni

Dk. Mwigulu Nchemba, Waziri wa Fedha na Mipango

Spread the love

 

RAIS Samia Suluhu Hassan amewaweka mtegoni Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Mwigulu Nchemba na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (TAMISEMI), Innocent Bashungwa baada ya kuwaagiza kupitia halmashauri moja moja kukagua namna zinavyokusanya mapato.

Agizo hilo limekuja siku chache baada ya Waziri wa TAMISEMI, kujinasibu kuwa wizara yake imevuka lengo la makusanyo ya mapato ya Sh bilioni 888.7 sawa na asilimia 103. Anaripoti Mwandishi Wetu, Mbeya … (endelea).

Hata hivyo, Rais Samia amesema anaamini kiwango hicho kingeweza kuwa kikubwa zaidi iwapo kungekuwa na ukusanyaji stahiki wa mapato hasa ikizingatiwa TAMISEMI inapewa fedha nyingi kutoka Serikali kuu.

Akizindua barabara ya Mbeya- Makongolosi – Chunya katika ziara yake mkoani Mbeya ambayo leo tarehe 6 Agosti ni siku ya pili, Rais Samia amesema pasipokuwepo na makusanyo ya kutosha Serikali haitakuwa na fedha za kutekeleza miradi ya maendeleo.

Amesema Halmashauri zinaomba pesa nyingi kutoka serikali kuu ila hazirudishi pesa nyingi kwa serikali kuu.

Amesema kwa kuwa sasa wilaya ya Chunya ilimezidi kufunguka anaamini upo uwezekano wa kukusanya pesa nyingi zaidi.

“Inawezekana pesa zinazokusanywa katika halmashauri hizo hazipelekwi vizuri hivyo nimewapa kazi Waziri wa fedha na TAMISEMI kazi ya kupita halmashauri moja moja kukagua halmashauri moja moja kuangalia jinsi wanavyokusanya mapato.

“Mapato mwaka huu ukusanyaji umekwenda vizuri kwa asilimia 103 lakini najua mnaweza kufanya zaidi, najua pesa nyingi zaidi zinapotea.

“Nimewapa kazi waziri wa fedha na Tamisemi na timu zao kuhakikisha halmashauri zinapanga malengo yanayokidhi ya kukusanya mapato na tunayaona serikali vinginevyo yale mabilioni mnayoyataka kutekeleza miradi mbalimbali hayatashuka kwenu kwa sababu yanapotea,” amesema.

Pamoja na mambo mengine amesisitiza wakazi wa wilaya hiyo kuitunza barabara hiyo pamoja na miundombinu mingine ili idumu kwa muda mrefu.

Waziri wa Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Innocent Bashungwa

“Miundombinu ni mali yenu, mkiiharibu mapema mtajiharibia wenyewe. Miundombinu hii imejengwa ili itumike kusafirisha watu na bidhaa ni wakati wetu.

“Tarehe nane tunafungua ruzuku ya pembejeo, mbolea, kuna fedha za vijana kwa kilimo cha umwagiliaji, tutafanya vyote ili barabara hii itumike kusaifirisha mazao kwa wingi kwa sababu sasa masoko kwa wakulima si tatizo, limeni unavyoweza hakikisha unaweka chakula cha kutosha kwa familia zenu, ziada uza popote,” amesema.

Awali Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Mhandisi Rogatus Mativila amesema barabara hiyo yenye urefu wa kilomita 39, imejengwa kwa gharama ya Sh bilioni 67.4.

“Bado ipo kwenye kipindi cha uangalizi hadi tarehe 21 Septemba mwaka huu,” amesema.

error: Content is protected !!