Friday , 29 September 2023
Home Gazeti Habari za Siasa Dk. Mwigulu awachambua Kikwete, Hayati Magufuli na Samia
Habari za SiasaTangulizi

Dk. Mwigulu awachambua Kikwete, Hayati Magufuli na Samia

Dk. Mwigulu Nchemba, Waziri wa Fedha na Mipango
Spread the love

 

WAZIRI wa Fedha na Mipango wa Tanzania, Dk. Mwigulu Nchemba, amewafananisha waliokuwa marais wa Taifa hilo, Jakaya Mrisho Kikwete na Hayati John Magufuli kama marefa wa mchezo, ambao kila mmoja alichezesha akitumia moja ya njano na mwingine akiwa na nyekundi. Anaripoti Nasra Bakari, DMC … (endelea).

Kikwete alikuwa Rais wa Tanzania kati ya mwaka 2005 hadi 2015, kisha akamwachia Hayati Magufuli kuanzia tarehe 5 Novemba 2015 hadi 17 Mach 2021, alipofariki dunia, katika Hospitali ya Mzena, Dar es Salaam.

Mara baada ya kifo hicho, aliyekuwa Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, aliapishwa kuwa Rais wa Tanzania, tarehe 19 Machi 2021, kumalizia ungwe ya awamu ya tano ya Hayati Magufuli.

Dk. Mwigulu aliwachambua Kikwete, Hayata Magufuli na Rais Samia, jana Alhamisi, tarehe 10 Juni 2021, bungeni jijini Dodoma, wakati akihitimisha hotoba yake ya Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2021/22.

Alianza kwa kusema, tangu Rais Samia alipoingia madarakani, ameonesha kukaa kwake katika nafasi mbalimbali kwenye Serikali za awamu mbalimbali Tanzania na Zanzibar, kumemfanya awe kiongozi aliyeandaliwa na kuiva na aliye tayari kuiongoza nchi kwa ufanisi mkubwa.

“Itakumbukwa mbali na nafasi zingine nyingi alizoshika katika miaka yake takribani ishirini Serikalini, Mama yetu (Rais Samia), amekuwa waziri katika awamu ya nne na amekuwa Makamu wa Rais katika awamu ya tano (ya Hayati Magufuli). “Kuna style za uongozi amejifunza,” amesema Dk. Mwigulu

“Kuna style za uongozi amejifunza” kupitia awamu hizo, alikopewa nafasi kuhudumu katika nafasi mbalimbali. “Mama yetu” alikuwa waziri katika awamu ya nne iliyokuwa ikiongozwa na Rais Jakaya Mrisho Kikwete.”

Rais Mstaafu Jakaya Kikwete

Akimwelezea Kikwete, Dk. Mwigulu amesema, “Kikwete alikuwa mzalendo wa kweli, alikuwa na maono, alikuwa mwalimu, alikuwa mzazi, alikuwa mlezi na kiongozi, alikuwa rahim sana, alikuwa mvumilivu sana aliyeamini kwenye mifumo, taasisi na Utendaji wa Kitaasisi.

Huku wabunge wakishangilia, Dk. Mwigulu amesema “hii naweza kuifananisha kama ‘refa kwenye mchezo’ wa mpira wa miguu, ambaye anachezesha mechi zake akiwa na ‘kadi ya njano tu’, kadi nyekundu anaiacha nyumbani.”

Amesema, katika utawala wa Kikwete, ukicheza rafu mara ya kwanza anakuonya kwa kukuelekeza, ukicheza rafu mara ya pili anakupa kadi ya njano, ukikosea anakupa kadi ya njano tena na alipotakiwa kutoa kadi nyekundu mara nyingi alionya kwa mdomo, kwa kuwa kadi nyekundu alikuwa anaiacha nyumbani.

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan

“Rais Kikwete aliamini sana kwenye mifumo na utendaji wa kitaasisi. Kwa mtazamo wangu, jinsi “Mama yetu” alivyoanza ni dhahiri amepata funzo kwenye awamu hiyo ikiwemo funzo la uzalendo, maono na kuamini kwenye “mifumo, taasisi na utendaji wa kitaasisi” na hapa naweza kusema ameichukua “kadi ya njano”, anayo na ameanza kutumia kama mnavyoona,” amesema.

Dk. Mwigulu akimchambua Hayati Magufuli amesema, “Mama yetu, alikuwa Makamu wa Rais katika awamu ya tano iliyokuwa ikiongozwa na Hayati Rais Magufuli.”

“Hayati Rais John Magufuli, alikuwa mzalendo wa kweli, alikuwa na maono, alijitoa kwa nguvu zote, alikuwa na uthubutu sana, mtu wa vitendo sana na muumini wa matokeo na kuchukua hatua za papo kwa papo.”

“Kama refa wa mchezo wa mpira wa miguu, alikuwa akienda kuchezesha mechi zake akiwa na “kadi nyekundu tu”, kadi ya njano alikuwa anaiacha nyumbani,” alisema Dk. Mwigulu huku wabunge wakishangilia.

“Ukicheza rafu mara ya kwanza tu anakupa kadi nyekundu, wakati mwingine hata asipoiona rafu yeye, mchezaji au shabiki akisema ameona rafu anakupa kadi nyekundu, hata mimi mwenyewe niliwahi kutembelewa na kadi nyekundu nikakosa michezo kadhaa.”

Huku wabunge wakiendelea kufurahia, alisema “Hayati Dk. Magufuli aliamini kwenye nidhamu ya hali ya juu ya mchezo. “Mama yetu” alikuwa Line one na Mheshimiwa Majaliwa akiwa Line two. Hivyo, “Mama yetu” amepata mafunzo kwenye awamu.”

Dk. Mwigulu akijikita kumwelezea Rais Samia alisema, “kuna style za uongozi amejifunza”. “Mama yetu” anazo kadi zote, “kadi ya njano” na “kadi nyekundu.”

“Mama yetu” ni Mzalendo wa kweli, ni Mwadilifu sana, ana Uthubutu, ana Maono, anaamini kwenye “Mifumo, Taasisi na Utendaji wa Kitaasisi” hataki maneno anataka vitendo,” alisema.

Rais John Magufuli akizindua kitabu cha Rais Mstaafu, Hayati Benjamin Mkapa, wengine ni wastaafu, Jakaya Kikwete na Ali Hassan Mwinyi

Waziri huyo, alitumia fursa hiyo kutoa rai “kwa watumishi wote wa umma na watanzania kwa ujumla tuchape kazi kwa bidii, kwa uadilifu na uzalendo mkubwa.”

“Kwa watumishi wa umma tusimamie matumizi ya fedha za walipa kodi kwa uadilifu mkubwa na kwa watanzania tulipe kodi bila shuruti.”

“Tabia moja ya refa asiyependa kuonea upande wowote, huwa hawezi kupendelea upande wowote,” alisema Dk. Magufuli na kuongeza:

“Kwenye michezo ya mieleka huwa mnapewa tahadhari ya don’t try this at home, kwenye maslahi ya nchi wanaotaka kumjaribu MAMA YETU nawaonya “Don’t try at all”. Tujiepushe na kadi Nyekundu.”

1 Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Kapinga: Usambazaji umeme vijijini mwisho Desemba 2023

Spread the love  NAIBU Waziri wa Nishati, Judith Kapinga, amesema ifikapo mwezi...

Habari za Siasa

Mgongano wa kimasilahi wamhamisha Chande TTCL

Spread the love  ALIYEKUWA Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO),...

Habari za SiasaTangulizi

Mgawo wa umeme: Rais Samia ampa miezi sita bosi mpya TANESCO

Spread the love  RAIS Dk. Samia Suluhu Hassan, amempa miezi sita Mkurugenzi...

Habari za Siasa

Rais Samia avunja bodi ya REA

Spread the loveRAIS Dk. Samia Suluhu Hassan, amemteua Balozi Jacob Kingu, kuwa...

error: Content is protected !!