September 27, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Dk. Mwakyembe: Tunafungua Ligi kwa tahadhari kubwa

Spread the love

BAADA Rais wa Tanzania, John Magufuli kuruhusu shughuli za michezo kuendelea kuanzia Juni Mosi, 2020, Waziri wa Habari, Sanaa, utamaduni na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe amesema kuwa wanaenda kufungua Ligi Kuu Tanzania Bara huku wakiwa na tahadhari kubwa. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).

Akitoa kauli hiyo mbele ya wanahabari jijini Dodoma, Mwakyembe amesema kuwa tayari Mkurugenzi wa michezo kutoka Wizarani, BMT na wataalamu wa Afya tayari wameshaanza vikao kuona namna gani wanaweza kuwapima wachezaji wote na kutoa muongozo wakati wa michezo hiyo.

“Sasa hivi  Mkuregenzi wangu wa Maendeleo ya Michezo, BMT na wenzao wapo kwenye vikao wakiwa wamewakaribisha wenzao wa Wizara wa Afya kuangalia wanafanyaje ili kuwapima wachezaji ili tuweze kuingiza wachezaji uwanjani waliotimamu,” alisema Dk. Mwakyembe.

Waziri Mwakyembe aliongezea kuwa hata kama wakishawapima wachezaji hao watalazimika kufuata taratibu zingine za kujikinga kama kunawa mikono kabla ya kuingia uwanjani, kutosalimia na kukumbatiana wakati wakushangilia bao.

Aidha katika hatua nyingine Mwakyembe ameeleza kuwa huenda Ligi hiyo ikachezwa katika kituo kimoja kutokana na timu nyingi za Ligi Kuu kuwa katika hali mbaya ya kiuchumi kwa kipindi hiki.

“Klabu zetu za michezo ya Mpira wa miguu zina hali mbaya kiuchumi ule utaratibu wa zamani timu kusafiri kwenda kwenye mikoa tofauti kucheza mechi hawatoweza, lazima tutambue hawana kipato kutokana Ligi kusimama,” aliongezea Waziri huyo.

Baada ya ruhusa hiyo klabu mbalimbali za Ligi Kuu zinatarajia kuanza maandalizi kwa ajili ya kumalizia michezo iliyosalia huku wakisubiri ratiba kutoka bodi ya Ligi na TFF katika kukamilisha msimu huu.

Ligi hiyo ilisimama machi 17, 2020 mwaka huu kutokana na mlipuko wa ugonjwa wa homa ya mapafu unaosababishwa na kirusi cha Corona, huku Simba ikiwa kileleni kwenye msimamo baada ya kukusanya alama 71 na Singida United kuburuza mkia ikiwa na alama 15, huku wakiwa wamesalia na michezo tisa katika kujinasua kushuka daraja.

error: Content is protected !!