January 19, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Dk. Mwaka anafungiwa, sangoma huria’

Baadhi wa wateja wa kiliniki ya ForePlan wakiwa nje ya jengo la kliniki hiyo baada ya kufungwa

Spread the love

MGOGORO unaoiandama Kliniki ya Foreplan, inayohudumia akinamama wanaohangaika kutunga mimba, umepanuka.

Awali ulikuwa umehusisha mmiliki wa kliniki hiyo, Dk. Juma Mwaka, na Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala, peke yao.

Lakini sasa, kwa yaliyotokea kufikia Jumanne jioni, Mahakama nayo imejikuta ndani ya mgogoro, kwa kulazimika tu kutumikia wajibu wake mkuu wa kusimamia haki.

Ilichokifanya ni kuchukua hatua ya kutetea maamuzi yake ya kisheria, ikitaka yaheshimiwe na kutekelezwa kwa ukamilifu wake.

Tatizo lilianza 6 Novemba, 2014, Baraza hilo, kupitia kwa Msajili wake, Mboni Bakari, lilipoifunga kliniki hiyo isitoe huduma kwa muda usiojulikana.

Kliniki hiyo ipo Bungoni, Ilala, Dar es Salaam, ikitoa huduma ya tiba mbadala kwa akinamama wenye tatizo la kutopata ujauzito, wengine wakiwa wamekosa ufumbuzi kwenye tiba za kisayansi.

Ni kwa sababu hiyo, hasa kwa vile tatizo hilo linawakabili wanawake wengi nchini, kiasi cha kuzaa tatizo jingine zito zaidi la kusambaratika ndoa nyingi, Foreplan imejipatia umaarufu mkubwa.

Gazeti hili lilishuhudia Ijumaa, Jumatatu na juzi Jumanne, umma wa wanawake, wakiwemo walioandamana na waume zao, wakisubiri huduma.

Ijumaa walikuta kliniki imefungwa na kushauriwa kurudi Jumatatu ikitarajiwa zitakuwa kawaida. Haikuwa. Walirudi Jumanne ambapo Dk. Mwaka aliahidi zingerudishwa.

“Ni kweli niliwaahidi wateja wetu kuwa leo (juzi Jumanne) wafike kupata huduma kwa sababu, nilitegemea wale watu watatii amri ya mahakama. Kumbe watu wenyewe hawana utii kwa sheria,” alisema.

Yalikuwa ni majibu ya Dk. Mwaka baada ya kuulizwa imekuaje watu waendelee kulalamika kukosa huduma wakati Jumatatu aliwaahidi huduma zingeanza tena Jumanne.

Uamuzi wa Baraza kufungia kliniki ya Foreplan, umechukuliwa kwa madai kuwa kliniki inafanya kazi kinyume cha Sheria ya Tiba Asili na Tiba Mbadala Na. 23 ya mwaka 2002.

Baraza limeorodhesha mambo tisa inayodai ni kasoro na kutaka zirekebishwe na mmiliki atoe taarifa atakapokuwa amerekebisha.

Hapo, baraza litafanya ukaguzi na tathmini, na likiridhika, huweza kufuta uamuzi wake.

Moja ya mambo hayo ni wafanyakazi waliopo kudaiwa hawakidhi vigezo na hawajasajiliwa.

Dk. Mwaka ambaye huzielezea huduma za kliniki yake kupitia vyombo vya habari, hakuridhika, akisema madai ni ya jumlajumla. Alikimbilia Mahakama ya Wilaya ya Ilala.

Alifungua madai yaliyosajiliwa kwa Na. 204/2014, yakiambatana na ombi la amri ya muda ya kusitisha utekelezaji wa uamuzi wa Baraza.

Hakimu Mkazi Msafiri baada ya kusikiliza hoja za Dk. Mwaka, ambaye aliwakilishwa na Wakili Ngasa Daja Mbonje, alitoa uamuzi wa upande mmoja, exparte, akisitisha kwa muda utekelezaji wa uamuzi wa kufungia kliniki.

Amri ya mahakama imepuuzwa. Kliniki imekutwa bado imefungwa. Kufuli zinaning’inia kwenye milango mpaka Jumanne jioni.

MAWIO ilishuhudia wateja wakipiga mayowe kulalamikia uamuzi huo, ambao wanasema unawaletea usumbufu na unyanyasaji.

Wakati kila mmoja akitafakari, huku wafanyakazi wakibaki na fadhaa, wasijue hatima, wakatokea watu wapatao wanane, wakiwemo askari wawili wa Polisi waliobeba bunduki. Msafara ulifika kwa gari Na. STK 4419 aina ya Land-Cruiser.

Polisi walisindikiza walioonekana ni wafanyakazi wa Wizara ya Afya ambao waliongeza kufuli za minyororo milangoni. Walifanya hayo bila ya kikwazo chochote. Wafanyakazi walizidi hofu.

Sinema ikapata kiungio. Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) akaomba aunganishwe kwenye kesi. Sasa si mgogoro wa pande mbili tu, Kliniki na Baraza la Tiba Asili. Serikali kuu ndani.

Mshangao. Amri ya Mahakama ya Wilaya haijatekelezwa. Wahusika wamejificha. AG anatinga kuwasimamia, pamoja na Kliniki kusisitiza wanawashitaki wahusika kwa ubinafsi wao.

Mahakamani Jumatatu, 17 Novemba, anakutwa hakimu mpya, Adolph Sachore, wahusika wanaelezwa Hakimu Msafiri amesafiri Mwanza.

Hakimu Sachore baada ya kusikiliza hoja za pande mbili, alisema mahakama imekubali AG aunganishwe; amri ya mahakama hiyohiyo ya kutaka walalamikiwa wakamatwe, imefutwa. Mahakama inatengua amri yake hata kabla ya kutekelezwa! Waliokaidi wamehifadhiwa. Sinema kabambe.

 

Wakili wa Dk. Mwaka kutoka Kamanija and Company Advocate, anapinga yote hayo.

“Hatujaridhika na uamuzi wa Mahakama. Unapofuta amri ya kukamatwa walalamikiwa kwa maana nyingine, sasa itatoka wapi nguvu ya kituo kufunguliwa?”

“Kwa kuwa hakuna aliye juu ya sheria, amri za mahakama lazima ziheshimiwe bila kujali wasifu wa mtu yeyote serekalini, lengo ni kudumisha hadhi ya Mahakama na utawala wa sheria. Bila sababu za msingi Mahakama inadharauliwa na yenyewe inajidharau… haki inapindishwa.

“Kama Dk. Mwaka ana mawakili wawili wanaomwakilisha mahakamani na bado ananyimwa haki, hali ikoje kwa masikini wasio uwezo wa kupata mawakili?”

Nassoro Amani, mkazi wa Tegeta, Dar es Salaam, anayekadiriwa kufikia umri wa miaka 60, ambaye amefika kliniki na wake zake watatu, alisema “wote wanataka watoto.”

“Tangu mwezi uliopita nimelipa hela, leo tumekuja kuchukua mavumba (dawa). Mke wangu mdogo nimemjengea kibanda Bunju, lakini hataki kukaa, anataka mtoto. Mimi naonekana siwezi.

“Tangu Ijumaa tunalia hapa tunakuja bila ya kupata huduma, tunaiomba serikali ikifungue kituo kwa sababu hatutibiwi kwa magendo, tunalipa hela halali na risiti tunazo,” alisema.

Mwanamke mwingine, Prisca Simon, anayeishi Buguruni, alisema wanawake wengi wameachwa kwa kukosa watoto kwenye ndoa zao. “Ukija hapa, kwa miezi mitatu ya kutumia dawa, unashika ujauzito, ndoa inatengamaa.

“Kitendo cha kumfungia Dk. Mwaka, tunajisikia vibaya sana. Huko mitaani wako masangoma hawafungiwi, gesti na mabaa yanayochangia maradhi hayafungiwi lakini Dk. Mwaka wanamfungia,” alisema.

“Kwenye ndoa usipopata mtoto, mwanamume anatoka nje. Anaweza kumpata huko, lakini wapo wanaokosa na wakirudi nyumbani wanapeleka maradhi. Mtu anakupa maradhi badala ya mtoto.

“Tunakuja kupata tiba. Hatuondoki hapa kwa sababu watoto wapo kwa Dk. Mwaka ukitumia tu dawa zake, unapata matumaini. Wakifungue kituo tuendelee kupata dawa,” anasema.

Maofisa walioorodheshwa kama walalamikiwa, ni Mboni Bakari, Dk. Liggle Vumilia, Dk. Mahewa Lusinde, Vera Nelson Ndechilio, Sophia Mtomole, John Chilomo, Laura Marandu na Dk. Jacqueline Kiloji.

Ripoti mpya ya Shirika la Afya Duniani (WHO) inasema karibu asilimia 80 ya watu wote duniani wanatibiwa kwa dawa asili. Kwa Tanzania, zaidi ya asilimia 60 wanaishi kwa kutegemea tiba hiyo.

Kumbukumbu zinaonesha Kliniki ya Foreplan inapokea hadi wahitaji 7,500 kwa mwezi.

error: Content is protected !!